Kesi ya mauaji ya Thomas Sankara yaanza miaka 34 baada ya kifo chake

Mahakama ya kijeshi Ouagadougou imeanza kusikiliza kesi inayowakabili watu 14 wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Thomas Sankara miaka 34 iliyopita.

0
Thomas Sankara, rais wa zamani wa Burkina Faso.

Mahakama ya kijeshi mjini Ouagadougou Jumatatu 11 Oktoba ilianza kusikiliza kesi inayowakabili watu 14 ikiwemo rais wa zamani wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kiongozi wa Burkina Faso, Thomas Sankara miaka 34 iliyopita.

Thomsa Sankara na wengine 12 walishambuliwa kwa risasi Oktoba 15, 1987 wakati wa mabadiliko ya siasa yaliyomleta uongozini aliyekuwa mwandani wake Blaise Compaore.

Compaore, mshukiwa mkuu wa mauaji hayo amesusia kesi hiyo.

Campaore aliongoza Burkina Faso kwa miaka 27 kabla ya kuondolewa madarakani 2014 baada ya machafuko na ghasia yaliyomfanya kuenda uhamishoni nchi jirani ya Ivory Coast alikopewa uraia.

Blaise Campaore, rais wa zamani wa Burkina Faso.

Yeye na mwandani wake Jenerali Gilbert Diendere, kwa wakati fulani aliongoza kikosi maalum cha usalama wa rais wanakabiliwa na shtaka la kushiriki katika mauaji,kuhatarisha usalama wa taifa na kuficha miili.

Diendere, mwenye umri wa miaka 61, anatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kula njama dhidi ya serikali ya mpito iliyochukua uongozi baada ya kubanduliwa uongozini kwa Blaise Campaore.

Mtuhumiwa mwingine katika mauaji hayo ni Hyacinthe Kafando, aliyekuwa mkuu wa usalama katika serikali ya Compaore.

Diébré Jean Christophe, daktari aliyetengeneza cheti cha kifo cha Sankara, ambacho kilionyesha kuwa rais huyo wa zamani alikufa kifo cha kawaida ni mtuhumiwa mwingine katika mauaji hayo na  anashitakiwa kwa kugushi waraka wa umma.

Thomas Sankara alikuwa kiongozi wa aina gani?

Thomas Sankara aliingia uongozini baada ya mapinduzi ya serikali mwaka wa 1983 akiwa na umri wa miaka 33. Alibadili jina la nchi kutoka Upper Volta jina lililotolewa na serikali ya ukoloni ya Ufaransa hadi Burkina Faso, jina linalomaanisha “nchi ya watu wanyoofu”.

Kati ya mabadiliko mengine aliyoleta ni pamoja na kupiga marufuku ukeketaji wa wanawake, ndoa za lazima na ndoa za mume mmoja na wake wengi. Alipiga marufuku matumizi ya madereva wa serikali na kuwazuia maafisa wa serikali kusafiri daraja la kwanza wanaposafiri kwa ndege.

Sankara mwenyewe aliishi maisha ya kawaida na hata kupunguza mshahara wake na ule wa wafanyakazi wa umma. Aliipa elimu kipaumbele na masuala mengine ya maendeleo.

Aligawa upya ardhi iliyokuwa ilkimilikiwa na mabwanyenye na kuwagawia wakulima wadogo, hatua hiyo iliongeza zao la ngano nchini humo.

Sankara alitoa wito wa kuwepo kwa Umoja wa Afrika dhIdi ya kile alichokiita “ukoloni mamboleo” wa taasisi kama vile Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.

Mjane wake Sankara anayeishi Ufaransa alikuja Burkina Faso katika ufunguzi wa kesi hiyo,Mariam ameishutumu Ufaransa kwa kupanga mauaji ya Thomas Sankara.

“Hii ni siku ambapo ukweli utajitokeza kwangu mimi binafsi, familia yangu na waBurkinabe”, alisema Mariam katika siku ya kwanza ya usikilizaji wa kesi hiyo.

Mariam Sankara, mjane wa Thomas Sankara
In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted