Mumewe Agnes Tirop ndiye mtuhumiwa mkuu wa mauaji yake

Mauaji ya mwanariadha wa Kenya Agnes Tirop huenda yalitokana na mzozo wa kimapenzi.

0
Agnes Tirop, mwanariadha wa Kenya

Mauaji ya mwanariadha wa Kenya aliyeiwakilisha nchi yake katika michezo ya Olimpiki mwezi Agosti Agnes Tirop huenda yalitokana na mzozo wa kimapenzi.

Mshindi wa medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 Agnes Tirop,alipatikana kauawa nyumbani kwake mtaa wa Rural Estate mjini Iten kaunti ya Elgeyo Marakwet siku ya Jumatano.

Polisi wanasema kuwa mumewe ambaye ametoroka ni mtuhumiwa mkuu katika mauaji hayo.

Agnes alishinda mbio za World Cross Country za 2015 na kushiriki mbio za mita 5,000 mjini Tokyo Japan katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka huu.

Wiki mbili zilizopitia, mwanariadha huyo aliyekuwa na umri wa miaka 25 wakati wa kifo chake, alikuwa nchini Ujerumani alikoshiriki katika riadha na kuibuka wa pili.

Mumewe Agnes alitoweka baada ya kuwapigia simu wazazi wa mkewe akilia na kuwaomba radhi kwa “kitendo alichofanya”.

Mkuu wa polisi eneo la Keiyo Kaskazini Tom Makori, amesema wanamska mumewe baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa yeye ni mtuhumiwa mkuu au anaweza kuwa na habari kuhusu mauaji ya mkewe.

Mwili wa Agnes ulipatikana umelowa damu kitandani mwake na ulikuwa na majeraha ya kisu shingoni.

Mkuu wa polisi Makori, anasema mahojiano na jamaa za Agnes yaliweka wazi kuwa mwanariadha huyo alikuwa na matatizo katika ndoa yake,mzozo ambao wazazi wake wanasema haukutatuliwa.

Kwasababu mumewe Agnes ametoweka na aliwapigia wazazi wake simu akilia na kuomba radhi, tunamtuhumu yeye kama mshukiwa mkuu wa mauji hayo.” Amesema Makori.

Kamera za CCTV na vifaa vingine vilikusanywa kutoka kwa nyumba ya Agnes ili kufanyiwa uchunguzi.

Makori anasema kuwa babake Agnes aliwapigia simu polisi siku ya Jumanne usiku kuripoti kutoweka kwa Agnes. Polisi walianza operesheni ya kumtafuta.

“Jumatano, wazazi walifika kituoni kufuatizia ripoti waliopiga na kuripoti kuwa mumewe Agnes aliwapigia simu akiomba radhi kwa kitendo alichofanya” Makori amesema.

Polisi ndipo walipoenda nyumbani kwake Agnes walipompata kauawa na mwili wake ulikuwa umelowa damu.

Mwanariadha mwingine mwanamke aliyekuwa rafiki wa karibu wa Agnes amewaambia polisi kuwa, Agnes na mumewe walikuwa wamegombana na Agnes alikuwa amehama nyumbani na kuenda kuishi kwenye kambi ya mazoezi iliyo mjini.

Mwanariadha huyo anasema, Agnes alilala kwenye kambi ya mazoezi Jumatatu na kuondoka Jumanne aliporudi nyumbani.

Mwanariadha mwingine amesema, walijaribu mara kadhaa kuwapatanisha Agnes na mumewe ila matatizo yaliendelea kukithiri.

Mshindi wa mbio za 800m Janet Jepkosgey na Selah Jepleting ni kati ya wanariadha waliofika nyumbani kwake Agnes.

Mumewe Agnes alikuwa  kocha wake ingawaje hakusafiri nae kuenda Tokyo Japan katika michezo ya Olimpiki,wandani wake wakisema mzozo wa ndoa uliongeza baada ya michezo hiyo.

Mwili wa Agnes ulipelekwa mochuari.

Rais Uhuru Kenyatta ameomboleza kifo cha Agnes Tirop akisema kifo chake kimekuwa pigo kubwa kwa riadha nchini, amewataka polisi kufanya uchunguzi na kuwamakata waliohusika na mauji ya Agnes Tirop.

Agnes Tirop

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted