VUTE NIKUVUTE YAIBUKA KESI YA MBOWE

Shahidi wa sita kutoka upande wa Jamhuri SSP Sebastian Madembwe, ametoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

0

Mbele ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, akifuatiwa na Halfan Bwire akiongozana na Mohamed Ling’wenya pamoja na Adamu Kasekwa wakiwasili Mahakama Kuu ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es salaam.

Kesi ya Uhujumu Uchumi yenye Makosa ya Ugaidi ndani yake imeendelea leo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambapo shahidi wa sita kutoka upande wa Jamhuri SSP Sebastian Madembwe, ametoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Kesi hiyo inamkabili mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu,ambao wanaidawa kula njama za kutenda vitendo vya kigaidi katika mikoa ya Arusha, Dar es salaam na Kilimanjaro.

Mrajisi wa leseni za bunduki kutoka Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kitengo cha Udhibiti na Usajili Wa Silaha za Kiraia, SSP Sebastian Madembwe, amedai silaha aina ya bastola, inayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa, haijasajiliwa. .

SSP Madembwe ametoa madai hayo mahakamani hapo wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, akielezea uchunguzi uliofanywa na kitengo chake dhidi ya silaha hiyo bastola aina ya Luger yenye Serial Number A5340.

SSP Madembwe amedai, tarehe 25 Novemba 2020, alipokea barua ya maombi kutoka Jeshi la Polisi, makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam, Idara ya Upelelezi, kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa silaha hiyo.

Amedai barua hiyo ilimtaka afanye uchunguzi wa taarifa za silaha hiyo ili kubaini kama inamilikiwa na mtu yeyote.

Baada ya kupokea maombi hayo alianza kufanya uchunguzi dhidi ya silaha hiyo, ambapo uchunguzi ulionesha haijasajiliwa katika kitengo chake.

Amedai, baada ya matokeo hayo aliindika barua ya kuonesha matokeo ya uchunguzi kwenda kwa mleta maombi akieleza kufuatia uchunguzi uliofanyika, matokeo yake yanaonesha silaha hiyo haijawahi sajiliwa.

Silaha hiyo aina ya bastola inadaiwa kuwa ya mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo, alikamatwa nayo tarehe 25 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kasekwa anadaiwa kumiliki silaha aina ya bastola, risasi tatu na maganda ya risasi, kinyume cha sheria.

Hata hivyo mvutano ukaibuka baina ya mawakili wa pande zote mbili kati ya mawakili wa Jamhuri na Utetezi, wakati amabapo shahidi huyo akiendelea kutoa ushahidi wake.Mvutano huo umeibuliwa na Wakili wa utetezi Jeremiah Mtobesya, aliyedai kuwa shahidi hana maelezo katika kifurushi cha committal, hivyo ushahidi wake hauwezi kuingia kwa mujibu wa kifungu cha 246 cha CPA.Mtobesya amedai kwamba ushahidi wake utaathiri mwenendo wa kesi hiyo kwa kuwa maelezo yake hayakuwamo katika kifurushi cha comittol hivyo washtakiwa hao hawakuyapata.

Baada ya kutoa pingamizi hilo, Wakili Hilla aliibuka na kuipinga akiiomba mahakana hiyo itupilie mbali akidai hoja hiyo ilitakiwa kutolewa katika mahakama ya chini ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kabla haijahamishiwa mahakamani hapo.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, alidai pingamizi hilo halina mashiko ya kisheria kwa kuwa lililetwa katikati ya ushahidi na kwamba walipaswa kuiibua mapema.

Wakili Kidando alidai, shahidi huyo aliorodheshwa tangu katika hatua ya awali na kwamba jina lake linasomeka namba 23 katika rekodi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mvutano ukaleta hoja nyingine za kisheria kutoka pande zote mbili, hali iliyofanya Jaji Tiganga, kuiahrisha kesi kwa muda wa dakika 15.

Kibatala: Samahani Mheshimiwa Jaji. Naomba kwanza kumwombea Wakili Jeremiah Mtobesya aweze kuingia kwenye orodha yetu, ambaye amechelewa kwa sababu nilizotoa mwanzoni. Baada ya hayo nitaomba sasa wakili Mtobesya aweze kusema alichotaka.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji, shahidi hana maelezo katika kifurushi cha committal.

Mtobesya: Kwa hiyo ushahidi wake hauwezi kuingia kwa mujibu wa kifungu cha 246 cha CPA. Hakuna maelezo yake, na nimeulizana na wenzangu kama upande wa mashitaka uliomba mwanzoni ombi lolote. Nimeambiwa hapana.

(Mahakama inakaa kimya).

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji, tutaomba pia maelekezo endapo wenzetu watafanya kwa usahihi, vipi kuhusu ushahidi ambao shahidi ameshaanza kuutoa hapa mahakamani.

Mtobesya: Na ninataatifiwa hapa na kaka yangu kwamba shahidi anatakiwa aondoke na ushahidi wake tuendelee na ushahidi mwingine kwa sababu hawawezi kupata faida baada ya sisi kusema kama wao hawakuomba mwanzoni.

(Mawakili wa Serikali wananong’onezana jambo).

(Jaji naye ameinama anaandika kidogo).

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji, ombi hilo halina mashiko yoyote ya kisheria.

Jaji: Maombi au pingamizi?

Wakili wa Serikali: Ahaaa! Pingamizi halina mashiko yoyote ya kisheria kwa sababu limeletwa katikati ya ushahidi wa PW6 kinyume na sheria. Na kama wangekuwa na hoja hiyo walitakiwa kufuatilia mapema. Lakini kwa wakili ambaye hakufuatilia tangu mapema proceedings hizi … Hoja yetu ya pili ni kwamba shahidi huyu aliorodheshwa tangu kipindi cha commital proceedings na anasomeka kama shahidi namba 23 tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Na hata katika barua yetu ya 11 Agosti 2021.

Jaji: Ukurasa wa ngapi?

Wakili wa Serikali: Ukurasa wa 32 na jina lake linaonekana namba 23.

Wakili wa Serikali: Labda lile neno S liondoke isomeke Sebastian. Lakini substance ilikuwa committed na ilisomwa katika mwenendo wa shauri hilo katika proceedings za tarehe 23 mwezi wa nane siku ambazo commital proceedings zilifanyika. Na jina lake limeandikwa Sebastian Madembwe SSP.

Wakili wa Serikali: Lakini pia katika ile list ya exhibit katika ukurasa wa 33 nyaraka inayokuja kuzungumzia imekuwa listed pale namba 18 ambayo pia imesainiwa na Sebastian Madembwe SSP nilikuwa committed na substance yake ilisomwa. Kwa hiyo kwa namna yoyote ile hatukutakiwa kuleta ombi kupitia kifungu cha 289 cha CPA ili shahidi huyu aweze kutoa ushahidi wake.

Wakili wa Serikali: Na tunasema pia matakwa ya Rule 8 Sub 2 ya The Economic and Organized Crime (Corruption and Procedure Rules ya 2016) takwa hili la kisheria lilitekelezwa na Mahakama. Iwe jina ama substance ya ushahidi anaotoa leo hii hakuna kitu kipya kama ambavyo wakili anajaribu kuonyesha Mahakama yako tukufu.

Wakili wa Serikali: Na kama hali iko hivyo hakuna haja ya kutoa amri yoyote ile kutokana na ushahidi ambao umetolewa na shahidi kwa sababu shahidi yupo sahihi kwa mujibu wa sheria. Hivyo Mheshimiwa Jaji tunaomba hilo pingamizi ulitupilie mbali ili shahidi wetu aweze kuendelea na ushahidi wake.

(Jaji anaandika kidogo).

Mtobesya: Kwanza kabisa wenzangu wameni- attack personally. Sikuwapo kwenye proceedings tangu mwanzo. Mimi kuchelewa kufika sidhani kunaweza kuathiri. Sisi tunachofanya hapa ni kuisaidia Mahakama kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria. Nimesema kwenye commital documents hakuna ushahidi wa shahidi huyu.

Mtobesya: Substance inaongelea mambo matatu. Kwanza ni majina, ingawa yamekosea hatuna shida na hilo, pili cheti atakachotoa na tatu hakuna kile ambacho “ataongea nini mbele ya Mahakama”. Tumeongea mara nyingi kuhusu hili kuwa kuna sababu ipo ya kumpatia mtu nyaraka za ushahidi kupitia commital. Na wasipokuwa wamefanya (hivyo) upo mlango mwingine wa wao kuomba kupitia kifungu cha 289 cha Criminal Procedure Act.

Wakili wa Serikali: Kama namwelewa Mtobesya anazumgumzia sasa kwamba documents kutosomwa.

Jaji: Kama nimekuelewa umesema haipo kwenye Commital Bundle.

Mtobesya: Nimesema haipo kwenye Commital Bundle, na kwa maana hiyo haijakidhi matakwa hayo ya kwenye 246 CPA.

Jaji: Umeridhika na line yake ya argument sasa?

Wakili wa Serikali: Hapana! Sikubaliani na Mtobesya. Yeye ana- argue kwamba haijasomwa. Maana akianza kujielekeza kwenye mengine na mengine inakuwa siyo sawa.

Jaji: Hoja yao ni kwamba u- argue kwa namna ambayo umeletea pingamizi.

Mtobesya: Kwa sababu haipo, ina maana haijasomwa, na kwa sababu haijasomwa, inakiuka sheria aliyosoma kaka yangu Kidando ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2016. Kingine kaka yangu anasema P. O imeletwa kinyume na sheria kwa sababu ilishapitwa. Hiyo siyo sawa. Jambo lolote linaweza kuibuliwa pale tu tunapoona tunaenda kinyume cha Sheria. Tunalo hilo jukumu kama wawakilishi wa wateja wetu na pia kama maafisa wa Mahakama.

Mtobesya: Kwa hiyo kama ilivyoombwa mwanzoni Mahakama itoe maelekezo na kukidhi matakwa ya Sheria. Na pia Mahakama ielekeze uwepo wa shahidi huyu. Sisi tunasema aondoke. Ni hayo tu kwa sasa Mheshimiwa Jaji.

(Jaji anainama na kuandika kidogo. Kisha ananyanyua kichwa na kusema).

Jaji: Nimesikia hoja zote. Naomba nipate muda na mimi.

Jaji: Nitapitia Sheria zote ambazo mmezitaja. Tutarudi tena saa tano na robo.

Jaji ananyanyuka na kuondoka.

Baada ya muda Jaji Joachim Tiganga akarejea tena mahakamani hapo ambapo uamuzi alioutoa ni kwamba Jaji Tiganga amesema ni msimamo wa sheria kuwa pale ambapo ushahidi unakuwa haujasomwa basi hauwezi kupokelewa mahakamani labda kama wataomba kama ilivyoelezwa na Wakili Mtobesya Kwenye Kifungu cha 289 CPA.

Amesema, jambo linalobishaniwa ni kwamba ushahidi haukusomwa hapa Mahakamani. Mahakama inayo jukumu la kukagua kama ushahidi ulisomwa au haukusomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Kisutu wakati wa commital inasoma.

Amesema, Mahakama wakati ina- examine records imeona kwenye ukurasa wa 21 kwamba maneno yafuatayo kwamba ushahidi na mashahidi yamesomwa kwa washitakiwa. Akasema Hakimu Simba tarehe 23 mwezi wa nane mwaka 2021.

Jaji Tiganga ameendelea kusema kuwa, akaorodhesha mashahidi 21 na jina la shahidi namba sita linaonekana katika ukurasa wa 31. Na kwamba mashahidi hao waliorodheshwa na maelezo yao yalisomwa mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Jaji Tiganga akihitimisha hoja hiyo amesema, kutokuwepo katika kifurusgi haimaanishi kwamba ushahidi wa shahidi namba sita haukusomwa.

“Hivyo Mahakama inaona pingamizi halina mashiko. Lengo la pingamizi ilikuwa ku- impeach record za Mahakama. Maelezo yaliyopo mahakamani yanaonesha kwamba ushahidi ulisomwa, hivyo naelekeza sasa shahidi aendelee,” amesema Jaji Tiganga

Mbali na Mbowe, katika kesi hiyo wengine ni, Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021, Mbowe anadaiwa kufadhili mipango ya kutekeleza ugaidi kwa kutoa fedha kwa washtakiwa wenzake.

KESI INAENDELEA

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted