Abdalla Hamdok: Maisha yake kabla na baada ya kubanduliwa madarakani

Baada ya wiki kadhaa za kifungo cha nyumbani, ambapo Sudan ilitikiswa na maandamano makubwa, alirejea rasmi serikalini chini ya makubaliano na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

0
Abdalla Hamdok,waziri mkuu wa Sudan

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok alikuwa kioo cha serikali ya mpito dhaifu nchini humo kwa zaidi ya miaka miwili kabla kuondolewa na kuzuiliwa katika mapinduzi ya mwezi uliopita na sasa amerudi uongozini.

Baada ya wiki kadhaa za kifungo cha nyumbani, ambapo Sudan ilitikiswa na maandamano makubwa, alirejea rasmi serikalini chini ya makubaliano yaliyotiwa saini na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kwenye hafla ilioneshwa kwenye televisheni.

Abdalla Hamdok ni mwanauchumi aliyeelimishwa nchini Uingereza na alifanya kazi katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya Afrika, alichonga taswira kama bingwa wa utawala bora na uwazi.

Aliibuka kama kiongozi wa kiraia wa Sudan baada ya wimbi la maandamano ya vijana ambayo hayajawahi kutokea yalimwangusha kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir, ambaye alikamatwa na jeshi mnamo Aprili 2019.

Hamdok hakuwa nchini Sudan na hakuhusika moja kwa moja na vuguvugu la maandamano lililomuondoa madarakani Omar al Bashir lakini uteuzi wa mwanateknolojia huyo ulishangiliwa na idadi kubwa ya watu na kupokewa vema na jumuiya ya kimataifa.

“Tukiwa na maono sahihi, tukiwa na sera zinazofaa, tutaweza kukabiliana na mzozo huu wa kiuchumi,” alisema baada ya kula kiapo chake cha kuongoza serikali ya mpito chini ya mkataba wa kugawana madaraka na majenerali.

“Ana ujuzi tunaohitaji zaidi kwa sasa,” Sumaila Ibrahim, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Khartoum, alisema wakati huo.

Lakini changamoto za Hamdok zilikuwa kubwa: msukosuko wa kisiasa na mzozo wa kiuchumi, uhaba wa bidhaa za kimsingi, na haja ya kujenga upya sekta ya benki wakati huo ikikaribia kuporomoka.

Kumhusu Abdalla Hamdok

Hamdok alizaliwa mwaka 1956 katika jimbo la Kordofan Kusini.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya shahada ya uchumi wa kilimo huko Khartoum alihamia mjini Manchester nchini Uingereza kwa masomo ya shahada ya uzamili.

Miaka kadhaa baadaye Sudan ilijipata kwenye mpaka wa kusini wa Sudan wakati Sudan Kusini ilipopata uhuru mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita na Sudan.

Kijiji chake mwenyewe kiligeuka kuwa eneo la vita na Hamdok alikuwa na nia ya kushinikiza kutatuliwa kwa migogoro ya wenyewe kwa wenyewe ya Sudan.

Hamdok alitumia uzoefu wake katika mipango mbalimbali ya Afrika ya kuleta amani wakati Sudan ilipotia saini mkataba na makundi ya waasi Oktoba 2020 ili kumaliza machafuko katika mikoa ya Sudan ya Darfur, Kordofan na Blue Nile.

Kabla ya kujiunga na serikali ya mpito  baada ya kuondolewa madarakani kwa Bashir alikuwa naibu katibu mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika mjini Addis Ababa.

Mnamo mwaka wa 2018 Hamdok alikataa ofa ya Bashir ya kuwa waziri wa fedha kama sehemu ya mabadiliko ya serikali.

Omar al Bashir, Rais wa zamani wa Sudan

Mageuzi yazua maandamano

Utawala wa Bashir kwa muda mrefu ulikuwa chini ya vikwazo vya Amerika lakini chini ya serikali ya Hamdok, Washington iliiondoa Sudan katika orodha ya wafadhili wa ugaidi.

Hilo na msamaha wa deni kutoka kwa wadai wa kimataifa ulifungua njia kwa uwekezaji wa kigeni.

Hatua hiyo ilileta mageuzi magumu ya kiuchumi, mengi yaliyokuwa yakiumiza  wa Sudan .Serikali yake ilifutilia mbali ruzuku ya petroli na dizeli.

Wasudan wengi waliona hatua hizo kuwa kali sana na maandamano dhidi ya serikali yalizuka katika maeneo kadhaa ya Sudan.

Ucheleweshaji wa kutoa haki kwa familia za waliouawa chini ya utawala wa Bashir, na hata wakati wa maandamano ya 2019 kufuatia kuondolewa kwa mbabe huyo wa kivita  ulimwacha Hamdok katika hatari ya kukosolewa.

Matatizo yake yaliongezeka kuanzia katikati ya mwezi Septemba wakati waandamanaji wanaoipinga serikali walipofunga bandari kuu ya Sudan, na kusababisha uhaba wa ngano na mafuta nchini kote.

Migawanyiko iliongezeka ndani ya Vikosi vya Freedom and Change, muungano wa kiraia ambao ulikuwa umeongoza maandamano dhidi ya Bashir, na ambao ulimchagua Hamdok kama waziri mkuu mnamo 2019.

Matatizo ya kisiasa na kiuchumi yalisababisha mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Burhan Oktoba.

Siku ya Jumapili 21 Novemba, Hamdok aliachiliwa kutoka kifungo cha nyumbani akitarajiwa kusaidia kuunda mustakabali wa nchi yake iliyokumbwa na migogoro.

Balozi wa kidiplomasia wa Norway, Therese Loken Gheziel, alionyesha imani yake kwake siku kadhaa kabla, akisema kwamba Hamdok “anaweza kuwa kiungo muhimu kuleta amani na uongozi wa kidemkrasia nchini humo.”

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted