Rais wa zamani wa DR Congo, Joseph Kabila atuhumiwa kwa ubadhirifu wa pesa.

Joseph Kabila na familia yake wanatuhumiwa kunyakua $138 milioni za serikali.

0
Joseph Kabila, Rasi wa zamani wa DR Congo.

Uchunguzi kuhusu aliyekuwa kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu madai ya ubadhirifu wa $138 milioni.

Uchunguzi wa mahakama umeanzishwa baada ya uchunguzi wa vyombo vya habari na nyaraka kumshutumu rais wa zamani wa DR Congo Joseph Kabila na familia yake kwa kunyakua dola milioni 138 za serikali, chanzo cha mahakama kilisema Jumatano.

Uchunguzi huo uliopewa jina “Congo Hold-Up”, na kuendeshwa na vyombo vya habari vya kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopinga ufisadi umeibua hasira kati ya wananchi humo katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Uchunguzi unamtuhumu Kabila, ambaye alitawala nchi hiyo kutoka 2001 hadi 2019 kwa ubadhirifu wa pesa kati ya 2013 na 2018.

Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema Jumatatu kwamba waziri wa sheria “alimwandikia mwendesha mashtaka mnamo Novemba 20,” siku moja baada ya uchunguzi kuanza kuchapishwa.

Waziri “alitoa amri kwa madhumuni ya uchunguzi na mashtaka,” Muyaya alisema.

“Sisi kama serikali hatuwezi kukaa kando baada ya tuhuma hizo kuibuliwa”

Chanzo katika ofisi ya mwendesha mashtaka katika Mahakama ya Cassation ikiwa ndio mamlaka kuu ya mahakama kilisema Jumatano kwamba “uchunguzi wa mahakama umefunguliwa” kufuatia ombi la waziri wa sheria.

Uchunguzi huo unakuja baada ya chombo cha habari cha uchunguzi cha Ufaransa cha Mediapart na Jukwaa la Kulinda Watoa taarifa kutoka Afrika, kupata hati milioni 3.5 kutoka Benki ya Kimataifa ya Gabon na Ufaransa (BGFI).

Vyombo vya habari kumi na tisa na mashirika matano yasiyo ya kiserikali yanayoratibiwa na Jumuiya ya Upelelezi ya Ulaya (EIC) yalitumia muda wa miezi sita kusoma nyaraka hizo.

“Nyaraka zinaonyesha kuwa rais wa zamani Kabila, familia yake na jamaa walipokea, kwa ushirikiano wa benki ya BGFI, angalau dola milioni 138 kutoka kwa hazina ya serikali kati ya 2013 na 2018,” Mediapart ilisema.

Uchunguzi ulibaini kuwa pesa hizo zilitwaliwa “kupitia kampuni bandia.”

Ofisi ya vyombo vya habari ya Kabila katika taarifa ilikataa “mashtaka ya uwongo” na kushambulia “unyanyasaji usio na msingi kutoka kwa mamlaka fulani ambayo imejificha nyuma ya vyombo vya habari.”

Benki ya BGFI, kutoka makao makuu yake katika mji mkuu wa Gabon Libreville, ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatano kwamba “imelaani vitendo vilivyo kinyume na sheria na maadili ambavyo huenda vilifanywa siku za nyuma ndani ya kampuni tanzu ya BGFI Bank RDC SA,” tawi la benki hiyo la Congo.



Benki hiyo iliongeza kuwa tangu 2018 “imechukua hatua muhimu za kujipanga upya” ikiwa ni pamoja na kuwasilisha malalamiko kwa ofisi ya mwendesha mashtaka.

Hata hivyo benki hiyo iliongeza kuwa ni jukumu la mamlaka za mahakama  kuthibitisha hatia kwa wale walioshtumiwa na“ina haki ya kumshtaki mtu yeyote anayeshiriki katika kusambaza na kutoa taarifa za uongo au kufichua habari za siri au za kibinafsi kwenye vyombo vya habari au kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.”
Umaskini umeenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, licha ya utajiri wake wa dhahabu, coltan, cobalt na madini mengine ya thamani ya juu. Mnamo mwaka wa 2018, karibu robo tatu ya watu waliishi chini ya $ 1.90 kwa siku, Benki ya Dunia inasema. Joseph Kabila alikua rais akiwa na umri wa miaka 29 tu mwaka 2001, baada ya babake Laurent-Desire Kabila kuuawa.

Hakushiriki uchaguzi wa Desemba 2018, ambao ulishindwa na kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Felix Tshisekedi ambaye alifanya kampeni kwa kiapo cha kukomesha ufisadi na kula rushwa. Ilikuwa ni kipindi cha kwanza cha mpito cha amani cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu nchi ilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Joseph Kabila rais wa zamani wa DR Congo
In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted