Shindano la Miss World 2021 laahirishwa baada ya Manasa Varanasi wa India na Wengine 16 Kukutwa na Covid

Tangazo hilo limetolewa Alhamisi, saa chache kabla ya hafla hiyo kuanza

0

Fainali ya Miss World 2021 imeahirishwa kwa muda baada ya washiriki kadhaa kuthibitishwa kuwa na Covid. Tangazo hilo limetolewa Alhamisi, saa chache kabla ya hafla hiyo kuanza. Washiriki kwa sasa wametengwa huko Puerto Rico, ambapo fainali ilipangwa kufanyika.

“Kwa kuzingatia kuongezeka kwa kesi za Covid kati ya washiriki, Shirika la Miss World limechukua uamuzi wa kuahirisha fainali ya Miss World,” ilisema taarifa rasmi.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya washiriki 17 na wafanyikazi kuthibitishwa kuwa na UVIKO-19. Miongoni mwa walioambukizwa ni Manasa Varanasi, ambaye alitawazwa Miss India World 2020, na alikuwa anaiwakilisha India kwenye shindano hilo.

“Tulikuwa na mashaka makubwa kwamba yeye (Manasa Varanasi) hangeweza kushiriki shindano hilo licha ya bidii yake kubwa na kujitolea kwake,  hata hivyo usalama wake ni wa muhimu sana kwetu,” Shirika la Miss India lilisema kwenye ukurasa wao rasmi wa Instagram.

“Tunasubiri kumkaribisha Manasa nyumbani, kumtunza na kumrudisha akiwa na nguvu, afya njema na furaha,” iliongeza. Fainali ya shindano hilo litafanyika upya katika jumba la Jose Miguel Agrelot Coliseum nchini Puerto Rico ndani ya siku 90 zijazo.

Miss World Organization ilisema kuwa uamuzi wa kuahirisha shindano hilo umechukuliwa baada ya mkutano na wataalam wa virusi na wataalam wa matibabu walioajiriwa kusimamia shindano hilo.

“Baada ya visa vya UVIKO 19 kuthibitishwa asubuhi ya leo baada ya kushauriana na maafisa wa afya na wataalam, uamuzi wa kuahirishwa ulifanywa,” bodi ya Miss World ilisema katika taarifa.

Washiriki wataruhusiwa kurejea nyumbani tu baada ya kuruhusiwa na maafisa wa afya.

“Hatua inayofuata kulingana na wataalam wa matibabu ni kuwekwa karantini mara moja, ikisubiri uchunguzi, na kufanya vipimo zaidi kulingana na hali kama hii. Washiriki na wafanyikazi wakiidhinishwa na maafisa wa afya na washauri kuwa wako salama watarudi katika nchi zao,” taarifa rasmi ilisema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted