Kenya yashinda tuzo ya World Travel Awards kama sehemu bora ya utalii barani Afrika

Hii ni mara ya saba mfululizo kwa Kenya kutambuliwa kama kituo kikuu cha utalii wa wanyamapori katika tuzo za WTA

0

Kenya inasalia kuwa kivutio kikuu cha utalii duniani kwa mwaka wa 2021, kulingana na tuzo za World Travel Awards.

Hii ni mara ya saba mfululizo kwa Kenya kutambuliwa kama kituo kikuu cha utalii wa wanyamapori katika tuzo kuu za kimataifa za kila mwaka.

Kenya ilizishinda Botswana, Afrika Kusini, Tanzania, Namibia, Zambia na Zimbabwe. Tangazo hilo lilitolewa Alhamisi wakati wa hafla ya tuzo za WTA, iliyofanyika kusherehekea ubora katika usafiri na utalii.

Shirika la ndege la Kenya Airways lilitambuliwa kama shirika linaloongoza barani Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii ya kenya Betty Radier alitaja ushindi huo kuwa ushahidi kuwa Kenya inatoa huduma bora katika sekta ya utalii.

“Kutambuliwa huku ni uthibitisho wa ubora wa Magical Kenya. Bila shaka ninaamini kwamba tutafanya bora zaidi.Tutaendelea na dhamira yetu ya kuhifadhi na kuonyesha kwa ulimwengu urithi wa kipekee wa wanyamapori ambao tumepewa kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema Betty Radier.

Wakati wa janga la UVIKO-19, vikwazo vya usafiri vilipoikumba sekta ya utalii, Wizara ya Utalii na Wanyamapori ilizindua kampeni kwenye mtandao kuonyesha wanyamapori katika mbuga na hifadhi kote nchini. Kampeni hiyo ilionyeshwa duniani kote kama sehemu ya kampeni ya Magic Awaits mnamo mwaka wa 2020.

Mnamo mwezi Agosti mwaka huu, Kenya ilishirikiana na mtandao wa kijamii TikTok ili kuonyesha kivutio kikubwa cha nyumbu wakivuka mto Mara katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.

“Kenya ni nchi yenye utajiri mkubwa na watu kutoka jamii nyingi tofauti, nchi yenye wanyamapori wakuvutia ambao tunataka kuangazia na pia kuwalinda… Bodi ya Utalii ya Kenya ina nia ya kuhakikisha MagicalKenya inasalia kuwa mstari wa mbele miongoni mwa watalii,” alisema Dkt Radier.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted