Shahidi akana kuhusika kumkamata Tito Magoti, Eric Kabendera na kupotea kwa Ben Saanane

Ni katika kesi ya Ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzanke watatu

0
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA.

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jana iliahirisha kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu mpaka siku ya Alhamisi Januari 13, 2022.

Jaji Joachim Tiganga ambaye anasikiliza kesi hiyo ameihirisha baada ya shahidi wa nane wa upande mashtaka, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilaya ya  Arumeru, Mrakibu wa Polisi (SP), Jumanne Malangahe kumaliza ushahidi na kuhojiwa na upande wa utetezi.

Shahidi huyo alianza kuhojiwa na Upande wa utetezi siku ya  Jumatatu Januari 10, 2022 ambapo siku hiyo upande wa utetezi hawakumaliza kumuhoji shahidi huyo na ukamuomba Jaji kuahirisha kesi hiyo ili kuendelea January 11 kwa kuwa muda ulikuwa umeshaenda huku upande huo ukidai kuwa bado ulikuwa na maswali mengi.

Mapema jana asubuhi  Wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala, alianza kumhoji shahidi huyo huku mengi yakiibuka ikiwemo suala la shahidi huyo iwapo alihusika kwenye suala la kumkamata mwanaharakati Tito Magoti, ambaye ukamatwaji wake ulielezwa kuwa ni kama utekaji nyara.

Wakili Kibatala alipomuuliza shahidi huyo juu suala hilo, shahidi alieleza kuwa hajawahi na wala hamfahamu Tito Magoti.

Shahidi huyo aliendelea kuieleza Mahakama kuwa Mbowe aliwapatia fedha za nauli Ling’wenya na wenzake  kutoka Morogoro kwenda Moshi kwa ajili ya kukutana nao ili waweze kupanga mikakati ya utekelezaji wa vitendo vya ugaidi.

Wakili Kibatala alipomuuliza tena shahidi huyo kuwa kwanini Mbowe alikawia kukamtwa kwa tuhuma za ugaidi ili hali taarifa zilishawafikia shahidi akaieleza Mahakama kwamba katika kipindi cha takribani mwaka mzima kulikua na mammbo mengi ya kiupelelezi ikiwemo wahalifu wengine waliosadikiwa kuhusika katika mpango huo.

Hata hivyo shahidi amekana Mbowe kukamatwa kutoka na madai ya Katiba mpya ambayo amekuwa akiizungumzia katika mikutano mbalimbali haswa kwenye kongamano la Katiba lililofanyika jijini Mwanza.

Upande wa utetezi ulipomliza kumuhoji shahidi huyo, wakili wa Serikali Robert Kidando, alisimama, na kuiambia Mahakama kuwa wanamaswali ya dodoso kwa shahidi kutokana na kile alichoulizwa na upande wa utetezi 

Katika maswali hayo ambapo shahidi aliongozwa na wakili Kidando alikiri kuwa sio kosa kwa mtu kutumiwa pesa ya nauli iwapo kama katumiwa kwa nia njema 

Sehemu ya mahojiano ya shahidi na Wakili wa Serikali Kidando

Kidando: Shahidi uliulizwa swali na wakili wa utetezi, kama ACP Kingai kama alikuwepo Agosti 9, 2020 kituo cha Polisi Mbweni na wewe ukasema hakuwepo elezea kwanini ulisema hakuwepo?

Shahidi: Tarehe hiyo ACP Kingai hakuwepo kituo cha Polisi Mbeni kwa sababu alikuwa kwenye kazi ya ufuatilia wengine.

Kidando: Uliulizwa kuhusiana na kukamatwa kwa Gabriel Mhina Agosti 19, 2020 na kufikishwa mahakamani Sepemba 31, 2020.

Shahidi: Alichelewa kufikishwa Mahakama katika tarehe hiyo kutokana na shughuli za kipelelezi.

Kidando: Mbowe alikamatwa kwa tuhuma zipi?

Shahidi: Kwa tuhuma za kigaidi na sio za kikatiba.

Kidando: Uliulizwa swali kuhusiana na mshtakiwa wa tatu (Ling’wenya) kufanya kazi ya VIP Protection na ukasema sio kosa kama mtu atafanya kwa nia njema na malengo mema, hapa ulikuwa inamanisha Nini?

Shahidi: Nilisema kufanya kazi ya VIP Protection sio kosa, kama mtu atafanya kwa nia njema lakini kama àtafanya kwa nia ovu hapo ndio kosa.

Kidando: Uliulizwa swali na wakili wa utetezi Dickson Matata kuwa kutumiwa nauli ni kosa au sio kosa na wewe ukasema sio kosa, kwanini ulisema sio kosa?

Shahidi: Sio kosa kama mtu atatumiwa kwa nia njema.

Kidando: SP Jumanne Uliulizwa siku ulipowakamata mshtakiwa wa pili na watatu kule Moshi na kuwafikisha kituo Kikuu cha Polisi Moshi na kuhusiana na kuandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu cha mahabusu( Ditention Register- DR)na ukasema mshtakiwa hawakuandikishwa katika kitabu hicho, hapo ulimaanisha Nini?

Shahidi: Mtuhumiwa au watuhumiwa wanaandikwa katika kitabu hicho pale tu anapokuwa ameshikiliwa na kuwekwa mahabusu ndio anaweza kuandikwa kwenye kitabu hicho (DR)

Kidando: Ulizwa swali katika bastola uliyoikamata kwa mshtakiwa wa Pili, kulikuwa na maeneo ambayo yangeweza kutoa alama za vidole ukasema ni kweli na ukasema ushahidi huo wa alama za vidole hukuleta Mahakama, hebu elezea kwanini ushahidi huo hukuleta Mahakama.

Shahidi: Utambuzi wa alama za vidole sikuleta mahakamani kwa sababu haukuwa na umuhimu wa kulinganisha nani alikuwa na hiyo silaha kwa sababu ilikamatwa kwa mshtakiwa huyo na hatukuwa na mashaka na kwamba utambuzi wa alama za vidole( Fingerprint) hufanyika kama tuna mashaka na mtu ndio huwa tunafanya ulinganishi.

Kidando: Mheshimiwa Jaji kwa upande wa mashtaka hatuna maswali mengine.

Shahidi pia alihojiwa na mawakili wa upande wa utetezi John Mallya na Peter Kibatala, ambao walihoji uhusika wake shahidi huyu katika utekaji na utesaji wa Eric Kabendera na Tito Magoti pamoja na kupotea kwa Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Freeman Mbowe

Sehemu ya mahojiano ya shahidi na wakili wa utetezi Mallya

Mallya: Vipi wshiriki wako katika kumkamata Kabendera?

Shahidi: Si kweli.

Mallya: Na wala hukwepo wakati anachukuliwa maelezo?

Shahidi: Sijafanya! Sijafanya! Sijafanya!

Mallya: Mshtakiwa Namba 4 alikuwa na Msaidizi wake anaitwa Ben Saanane alikamatwa na Mamlaka za Serikali ukiwa ofisa katika Ofisi ya DCI

Shahidi: Mie sijui lolote

Mallya: Lakini ulisikia kuwa Ben Saanane amepotea..?

Shahidi: Nilisikia kwenye vyombo vya habari

Sehemu ya mahojiano ya shahidi na wakili wa utetezi Kibatala

Kibatala: Upelelezi gani unaujua wewe zaidi ya kutesa vijana wa watu ambao walitumikia Nchi na Jeshi?

Shahidi: Sijatesa mtu mimi

Kibatala: Nakuuliza hapa chini ya kiapo, unamjua Tito Magoti au humjui?

Shahidi: Simfahamu Tito Magoti kabisa

Kibatala: Nikimleta hapa mahakamani kama shahidi akisema kuwa ulishiriki kumteka je?

Shahidi: Mie sijawahi kumteka

Kibatala: Na je unasemaje juu ya taarifa kuwa wewe ni miongoni wa watu wasiojulikana na umeshiriki kuteka na kutesa watu?

Shahidi: Hapana Mimi sijawahi kuteka mtu mimi

Pande zote za mawakili hawakuwa na maswali ya ziada kwa shahidi huyo, na hivyo kwa pamoja waliomba mahakama ihairishe kesi hiyo hadi Alhamisi, January 13.

Hata hivyo baada ya kesi kuahirishwa, mwandishi Kabendera aliandika kupitia mtandao wa Twitter kuwa hatasahau sura ya shahidi huyo Mrakibu wa Polisi (SP), Jumanne Malangahe huku akinukuu ujumbe wa Martin Maranja kuhusu uhusika wa shahidi katika utekaji.

Ujumbe wa mwandishi wa habari Eric Kabendera kupitia mtandao wa Twitter

Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, hivi sasa yuko mahabusu kwa zaidi ya siku 170 akituhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi  na ugaidi ndani yake.

Katika kesi hiyo Mbowe anadaiwa kupanga njama ya vitendo vya ugaidi na nia ya kuwaua viongozi wakuu wa Serikali. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mohamed Ling’wenya, Halfan Bwire na Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo wote wakiwa wastaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), wakitokea kikosi cha Makomandoo cha KJ 92 Ngerengere.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted