Bilioni 130 kutengwa kwa ajili ya kukabiliana na ukame

Serikali imesema itatenga fedha hizo kwa ajili ya kuchimba visima na kujenga mabwawa

0

Serikali imesema ina mpango wa kutatua changamoto ya ukame kwa kutenga shilingi bilioni 130 kwa ajili ya kuchimba visima, kukarabati na kujenga mabwawa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Abdallah Ulega hii leo alipofika katika Wilaya ya Kiteto kuwapa pole wakulima waliopoteza idadi ya Ng’ombe 1874 ambao wamekufa kutokana na kukosa maji na chakula.

Akizungumza na Wananchi wa Wilaya hiyo katika Tarafa ya Makame, Ulega amesema tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji imeshatenga kiasi cha shilingi  bilioni 130 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo huku akiwataka wataalamu wa mifugo kutoa elimu kwa wakulima kuhakikisha wanajikita kupanda majani na kuyavuna ili yahifadhiwe kwa ajili ya chakula pindi hali ya ukame itakavyojitokeza.

” Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inajali wananchi wake ndio maana tuliposikia kuwa Ndugu zetu mmepoteza Mifugo yenu tumefika kwa wakati kuwapa pole, ni agizo langu kwa wataalamu wa Mifugo kutoa elimu kwa Wakulima kuanza kupanda majani ambayo tutawaletea sisi ambayo yatasaidia chakula kwa Mifugo pindi ambapo hali ya ukame itapojitokeza” amesema Ulega na kuongeza 

“Nimefika hapa Makame Kiteto na kushuhudia hali ya mizigo ya Mifugo ambayo imekufa kwa kukosa Maji na Chakula, niwatoe hofu tayari Serikali ya Rais Samia imeshatenga shilingi bilioni 130 kwa ajili ya kujenga visima na kukarabati mabwawa ya kunyweshea Mifugo maji hasa katika maeneo yaliyoathirika na ukame na Kiteto ni mojawapo ya maeneo hayo, niwatake wataalamu wetu wakiwemo wahandisi kubainisha maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele haraka iwezekanavyo,” Amesema Naibu Waziri Ulega.

Amesema katika kuhakikisha wafugaji wanaondokana na vifo vingi vya Mifugo na kukabiliana na uhaba wa mifugo, Serikali itasambaza nyasi za malisho kwa Mifugo kwa ajili ya wafugaji kuzipanda na kuvuna ili kuhifadhi na kuzitumia wakati wa ukame na msimu kama huu.

Naibu Waziri Ulega pia ametumia fursa ya ziara hiyo kuwataka wafugaji kuacha ufugaji wa mazoea na kuanzisha ufugaji wa mavuno ambao utawasaidia wafugaji wote Nchini kufanya biashara ya Mifugo ambayo itawasaidia kusomesha watoto wao, kujenga nyumba zao pamoja na mazizi bora ya mifugo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted