Ma-RC wapewa siku 14 kutoa taarifa za halmashauri zao

Ni zile halmashauri ambazo zimeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato

0
Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa

Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa ametoa siku 14 kwa wakuu wa mikoa nchini kupeleka taarifa za halmashauri zao ambazo zimeshindwa kufikia malengo katika makusanyo ya mapato kwa kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu katika maeneo yao.

 Agizo hilo amelitoa leo jijini Dodoma,  wakati akitoa taarifa za mapato na matumizi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021.

Kwenye taarifa za makusanyo hayo Halmashauri ya Hanang’, imeongoza kwa kundi la halmashauri huku Kahama ikiongoza kundi la Manispaa, Mbulu kwa kundi la miji na Tanga imeongoza kwa Majiji.

Miongoni mwa maeneo wanayotakiwa kutolea taarifa ni kwa nini Wakurugenzi wa halmashauri zao wameshindwa kufikia malengo ya makusanyo na waeleze mikakati yao namna gani wanatoka walipo.

Wakuu wa mikoa katika maeneo husika naagiza ndani ya siku 14 kuanzia leo wawe wametoa taarifa Kwa Katibu Mkuu wa Tamisemi kwa mapungufu hayo pamoja na mapendekezo ya nini kifanyike,” amesema Bashungwa.

Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri huyo kutoa taarifa ya mapato kwa halmashauri kuingia katika wizara hiyo ambapo, amesema kipimo kwa Wakurugenzi kitakuwa ni makusanyo na matumizi kwa maeneo yao.

Aidha amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara hiyo kukamilisha mifumo yote inayohusu malipo na makusanyo ili ifikapo Julai Mosi 2022 ianze kutumika kwa lengo la kuondoa malalamiko na mapungufu.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted