Kenya: Vyama vya kisiasa na miungano ya kisiasa

Makubaliano ya kisiasa yamekuwa ya kawaida miongoni mwa wanasiasa katika kipindi chote cha baada ya ukoloni.

0
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Mnamo Machi 9, 2018 Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kiongozi wa upinzani mkuu, Raila Odinga, waliwashangaza wafuasi wao walipoweka tofauti zao za muda mrefu kando na kusalimiana mbele ya wakenya na kukubaliana kufanya kazi pamoja.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa wapinzani wa kisiasa Kenya kufanya mapatano ili wafanye kazi pamoja.

Makubaliano ya kisiasa yamekuwa ya kawaida miongoni mwa wanasiasa katika kipindi chote cha baada ya ukoloni.

Kenyatta na Odinga walikuwa wamehitimisha mapatano hapo awali. Odinga aliungana na rais wa zamani Mwai Kibaki baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Rais Kenyatta naye aliunda muungano wa Jubilee na aliyekuwa mpinzani wake William Ruto, na wakashinda uchaguzi wa 2013.

Hata hivyo, Uhuru na Raila kuweka tofauti zao kando na kuamua kufanya kazi pamoja kuliwashangaza wengi kwa sababu hakukuwa na upatanishi wa wazi uliofanyika.

Kabla ya wawili hao kupatana, chama cha upinzani cha Odinga, National Super Alliance, kiliongoza maandamano ya kupinga kutangazwa kwa Uhuru Kenyatta kama mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.

Uchaguzi wa kwanza ulifanyika Agosti 2017, na Raila Odinga akapinga matokeo ya uchaguzi huo akidai kulikuwa na wizi mkubwa wa kura.

Mahakama ya Juu ilibatilisha uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka IEBC iliyomtangaza Uhuru Kenyatta kama mshindi wa uchaguzi huo, na kuamuru uchaguzi mpya kufanyika baadae mwaka huo mwezi Oktoba 2017.

Lakini hata marudio hayo yalikataliwa na Odinga na chama chake cha National Super Alliance. Walipinga urais wa Kenyatta na Januari 30, 2018 Raila Odinga akaapishwa kama rais wa Wananchi.

Muungano wa NASA ulijumuisha vyama kutoka maeneo tofauti ya nchi vikiongozwa na viongozi kutoka maeneo hayo.

Miezi michache baada ya Raila Odinga kuapishwa kama rais wa wananchi, aliweka tofauti zake kando na kusalimiana na Uhuru maarufu “Handshake” kama ishara ya kumaliza miaka mingi ya uhasama kati yao.

Waliidhinisha mfumo wa kushughulikia changamoto za utawala ambazo zimechangia siasa za migawanyiko na uadui wa kikabila.

Mfumo huo uliitwa Building Bridges Initiative.

Kuja pamoja kwa viongozi hawa wawili kumemaliza mzozo wa kisiasa wa muda mrefu.

Washirika wa kisiasa wa viongozi hao wawili walianza kushirikiana. Hii ilijumuisha wawakilishi wao katika Bunge la Kitaifa na Seneti, ambapo washirika wa Odinga waliunga mkono sera za serikali.

Kwanini wahasimu hawa wajadi waliamua kuja pamoja na kuweka tofauti zao kando?

Mpango wa BBI ikiwa ndio mchakato uliochukuliwa na viongozi hawa wawaili ili kukomesha uhasama unaeleweka vyema kwa kutambua kwamba siasa za Kenya kimsingi zimechongwa na ushindani kati ya miongoni mwa vigogo wa kisiasa na makabila yao.

Viongozi wa kikabila wanaoshindana wana mamlaka na udhibiti usio rasmi juu ya makabila yao. Hutumia umaarufu wao kwenya makabila yao ili kuendeleza maslahi yao ya kiuchumi na kisiasa na pia kujadili mgawanyo wa madaraka na rasilimali.

Ubabe wao katika kutetea jamii na kabila zao na kujali maslahi yao ndio husababisha kuundwa kwa miungano ya kisiasa.

Mara nyingi muungano utakaoshinda uchaguzi huhakikisha kuwa walioshindwa hawapati usemi wala nafasi za uongozi.

Lakini wale waliotengwa wanaweza kusababisha uundaji wa mapatano mapya ikiwa mienendo mipya itasababisha kujumuishwa kwao katika mipango ya mamlaka na serikali.

Idadi ya watu kutoka makabila tofauti nchini na mfumo wake wa uchaguzi huchangia hali hii ya watu kutoka makabila machache kuendelea kuongoza.

Kenya ina makabila makubwa matano ambayo yanajumuisha takriban 65% ya watu wote.Katiba ya Kenya pia inawataka wagombea urais kushinda uchaguzi kwa 50% na kura moja na kifungu hiki kinalazimisha uundaji wa miungano.

Matokeo yake ni kwamba makubaliano yanavunjwa – na kujengwa – kwa msingi wa kuunda muungano bora utakaohakikisha ushindi katika uchaguzi.

Makabila hayo makubwa ni , Kikuyu kabila lake Rais Kenyatta,Luo lake Raila Odinga, Kalenjin lake William Ruto ,kuna Kamba na Luhya. Jamii ya kikuyu ikiwa kubwa zaidi kuliko makabila mengine na kumekuwa na marais wa tatu kutoka kabila hilo. Rais wa kwanza Jomo Kenyatta aliyeongoza Kenya baada ya kuondoka kwa mkoloni mwaka wa 1963. Kisha Mwai Kibaki kati ya 2007 hadi 2013, na baadae mwanawe Rais wa kwanza wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Jamii ya pili kubwa kwa idadi ya watu ni jamii ya Kalenjin, yake William Ruto. Rais wa pili wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi alitoka katika jamii hii. Rais Moi aliongoza kwa kipindi kirefu zaidi kutoka mwaka wa 1978 hadi 2002.

Makubaliano kati ya Raila na Uhuru Kenyatta katika Mpango BBI ulichangia kusambaratika kwa uhusiano kati ya Uhuru na naibu wake William Ruto.

Wawili hao waliweka mapatano kwa madhumuni ya kushinda uchaguzi wa 2013.Lakini baada ya Kenyatta kushinda uchaguzi uliokumbwa na utata wa 2017 na kuanza muhula wa mwisho wa uongozi, mapatano haya yalikuwa yamekwisha madhumuni yake.

Kenyatta alikuwa uongozini na naibu wake katika muhula wa kwanza lakini baada ya kushinda uchaguzi wa 2017 alianza kujilimbikizia mamlaka kwa kuondoa majukumu ambayo yalimuonyesha Ruto kuwa rais mwenza wa Uhuru.

Katika muhula wa kwanza, Ruto angewateua wandani wake katika nyadhifa mbalimbali serikalini.Pia aliratibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya serikali kote nchini.

Ruto pia alianza kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa miongoni mwa Wakikuyu kutoka jamii ya Kenyatta na makabila washirika katika eneo la Mlima Kenya.Wafuasi wa Kenyatta walitafsiri hili kama kudhoofisha udhibiti na mamlaka ya Kenyatta kwa jamii yake ya kikuyu.

Zaidi ya hayo, ongezeko la viwango vya rushwa katika miradi ya maendeleo ya serikali likawa suala la kutia wasiwasi. Wengi wa wafuasi wa Kenyatta walimshutumu Ruto na washirika wake kwa kujilimbikizia mali kwa madhumuni ya kufadhili kampeni zake za urais 2022. Walimshtumu Ruto kwa kutumia miradi ya maendeleo ya serikali kuonyesha kuwa ni yeye aliyeiwezesha.

Kenyatta alimgeukia Odinga kwa mapatano mapya ya kukata ushawishi wa kisiasa wa Ruto na kumaliza maandamano na vurugu ambayo yalipinga uhalali wake.

Huku baadhi wakimuona Kenyatta kuwa rais aliyechaguliwa kihalali, wengine walimwona hana uhalali. Hili pia lilimhusu Odinga ambaye ingawaje alitawazwa kama Rais wa Watu, alikosa mamlaka rasmi ya kutawala.

Hii ilikuwa kweli hata katika maeneo ya upinzani.Kwa kukosa uwezo wa kuendeleza miradi ya serikali na bila udhibiti wa taasisi yoyote, Odinga hangeweza kutoa manufaa yoyote kwa washirika wake, ambao wengi wao waliunga mkono upinzani kwa matumaini kwamba watafaidika iwapo wataingia madarakani.

Kilichokubaliwa katika BBI

Mapendekezo hayo yalikusudiwa kuoanisha maslahi ya wanasiasa ili kuhakikisha uwiano. Yalionekana kulenga kuhakikisha kuwa jamii kubwa zaidi za kikabila zinapata uwepo katika serikali kuu ya kitaifa. Walioshindwa pia wangepata wadhifa na kuwa na usemi bungeni.

Mapendekezo ya BBI yalikuwa:

Mapendekezo ya marekebisho ya katiba ili kupanua mamlaka ya kitaifa kwa kujumuisha wadhifa wa waziri mkuu miongoni mwa mengine.

• Pendekezo la kuanzisha nafasi ya kiongozi wa upinzani rasmi ambayo ingeshikiliwa na mshindi wa pili wa uchaguzi wa urais. Kiongozi wa upinzani angekuwa mbunge kwa wadhifa wake wa zamani.

• Mapitio ya mfumo wa uchaguzi ili kukuza usawa wa uwakilishi na usawa wa uraia kupitia uwakilishi sawia. Kenyatta na Odinga wametafuta uungwaji mkono kwa mpango huu kutoka kwa makabila mengine.

Mipango hii mipya inakusudiwa kupata usaidizi kutoka kwa bunge.Mpango huo ulitafuta kupata uungwaji mkono na wananchi kwa sababu baadhi ya mapendekezo yanahitaji kura ya Wakenya katika kura ya maoni. Kenya ina historia mbaya ya kura za maoni. Katika kura ya maoni iliyofanyika mwaka 2005 na nyingine mwaka 2010 ilileta mgawanyiko nchini. Moja ya kura hiyo ya maoni ilikuwa ya kurekebisha katiba ya 2010.

Ruto anaonekana kutengwa na mipango ibuka ya mamlaka. Yeye na washirika wake tayari wamepinga Mpango wa BBI kwa kusema kwamba mapendekezo yake yananuiwa kuwanufaisha matajiri badala ya wapiga kura na maskini kama yeye.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted