Amerika yashutumu amri ya nyuklia ya Putin, ikisema vikosi vya Urusi vimekumbana na matatizo

Kulingana na taarifa ya Pentagon, jeshi la Urusi halijafikia malengo ambayo lilikuwa limejiwekea kabla ya kuvuka mpaka na kuingia Ukraine.

0
Jeshi la Urusi

Amerika ilishutumu vikosi vya nyuklia vya Rais wa Urusi Vladimir Putin Jumapili, na kusema vikosi vyake vya kawaida vya ardhini vinakabiliwa na matatizo ya vifaa katika uvamizi wao wa Ukraine.

Maafisa wa Amerika walisema tangazo la kustaajabisha la Putin la kujitayarisha kwa mashambulizi ya nyuklia siku nne baada ya jeshi lake kushambulia Ukraine, lilikuwa la hatari na ni sehemu ya mtindo wa kubuni visingizio vya kuhalalisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.

Putin alisema alichukua hatua hiyo kujibu hatua za ‘uchokozi’ na ‘zisizo za kirafiki’ za NATO na nchi za Magharibi, huku mzozo wa Ukraine ukizidi kuwa mbaya.

“Huu ni mtindo ambao tumeuona kutoka kwa Rais Putin wakati wa mzozo huu, ambao ni kutoa vitisho ambavyo havipo ili kuhalalisha uvamzi zaidi.” katibu wa habari wa Ikulu ya White House Jen Psaki alisema.

Afisa mkuu wa ulinzi wa Amerika, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema hatua ya Putin ilikuja huku vikosi vya Ukraine, vikisaidiwa na silaha kutoka nchi za Magharibi, vikiendelea kuzuia majeshi ya Urusi kusonga mbele. Afisa huyo alisema kuwa vikosi vya Urusi vimekumbwa na matatizo ikiwemo usambazaji wa mafuta na matatizo mengine ya vifaa.

“Tunaamini kwamba hii sio tu hatua isiyo ya lazima kwake kuchukua, lakini ni hatua ya kuongeza mzozo huo,” afisa huyo alisema kuhusu tangazo la nyuklia la Putin.

“Tangazo lake halistahili kwasababu Urusi haijawahi kuwa katika hatari ya mashambulizi ya kinyuklia kutoka nchi za Magharibi, na NATO na hakika haikuwa chini ya tishio lolote kutoka kwa Ukraine,” afisa huyo alisema.

“Hatua yake inahatarisha zaidi hali ilivyo kwa sasa kwa sababu ni wazi kwamba kuna uwezekano kuwa uamuzi wake unaweza kufanya mambo kuwa hatari zaidi.”

Afisa huyo wa ulinzi wa Amerika alikataa kusema iwapo majeshi ya nyuklia ya Amerika, ambayo ni ya pili kwa ukubwa duniani, yamewekwa katika hali ya tahadhari.

“Tunasalia tu na ujasiri katika uwezo wetu wa kujilinda sisi na washirika wetu.”

Afisa huyo wa Amerika alisema Urusi sasa imetuma nchini Ukraine takriban theluthi mbili ya wanajeshi wake 150,000 iliowaweka kwenye mipaka ya nchi hiyo.

Lakini, kulingana na taarifa ya Pentagon, jeshi la Urusi halijafikia malengo ambayo lilikuwa limejiwekea kabla ya kuvuka mpaka na kuingia Ukraine.

Mpango wa Urusi wa kuiteka haraka miji miwili mikubwa zaidi ya Kyiv na Kharkiv, umedorora kwa sababu ya upinzani wa “kibunifu kutoka kwa wanajeshi wa Ukraine na Warusi.”

Kando na baadhi ya vitengo vya uchunguzi vinavyoonekana kuingia Kyiv, ambako vilijihusisha na mapigano, jeshi kuu la Urusi bado limekwama karibu kilomita 30 kaskazini mwa mji mkuu.

“Hawajaweza kutimiza kile tunachoamini walikusudia kutimiza kufikia siku ya nne. Ratiba yao iko nyuma.” afisa wa utetezi alisema.

“Hatujui kama ni kwa kushindwa kupanga vyema. Hatujui kama ni kushindwa katika utekelezaji” afisa huyo alisema.

Hata hivyo, afisa huyo alisema bado kuna theluthi moja ya jeshi la Urusi la uvamizi kwenye mpaka linalosubiri kuingia Ukraine.

“Hiyo ni nguvu kubwa ya vita.” afisa huyo alisema.

Afisa huyo alisema vikosi vya Urusi vinaonekana kujiandaa kuizingira miji ambayo haijaiteka kwa haraka, haswa Chernihiv kaskazini mashariki mwa Kyiv, na kuweka idadi kubwa ya raia katika maeneo hayo hatarini.

Ili kuhakikisha kuwa mji umetekwa kwa mafanikio, afisa huyo alisema,” majeshi hulenga miundombinu ya kiraia na kusababisha madhara kwa raia.”

“Hiyo inatia wasiwasi mkubwa” afisa huyo alisema, huu ndio mwanzo wa mbinu zilizokoseka za Warusi.”

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted