Wahamiaji haramu 55 watiwa mbaroni mkoani Katavi

Pia kati ya wahamiaji hao, saba bado wanafanyiwa uchunguzi uraia wao na kwamba wamekamatwa kupitia doria endelevu.

0

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Katavi nchini Tanzania, imewakamata wahamiaji haramu 55, ambao kati yao 48 ni raia wa Burundi, wakiwemo watoto wanne.

Watoto hao walikuwa wakisoma shule ya msingi Luhafwe wilayani Tanganyika na Muungano Manispaa ya Mpanda mkoani humo.

Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Katavi, Vicent Haule, amesema wanaendelea na mchakato wa kuwarejesha makwao wahamiaji hao, huku raia wengine 15 wa Burundi wote wanaume wanatarajia kufikishwa mahakamani.

Pia kati ya wahamiaji hao, saba bado wanafanyiwa uchunguzi uraia wao na kwamba wamekamatwa kupitia doria endelevu.

“Tumewakamata maeneo ya Ikola na Luhafwe wilayani Tanganyika na wengine Mpanda Mjini, watatu wametokea kambi za Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma,” amesema Haule.

Mbali na hilo Haule amesema inavyoonekana kuna wimbi la Watanzania waliopata uraia, wanachukua ndugu zao kutoka Burundi kwa lengo la kuja kuwasomeshea watoto wao kupitia fursa ya elimu bure pasipo kufuata utaratibu.

“Tumekuta wanafunzi wanne shule ya msingi Luhafwe wilayani Tanganyika na Muungano katika Manispaa ya Mpanda wanakuja kusoma kwa kutumia mgongo wa elimu bure, wanachukua kama fursa ya kuja hapa kusoma bure hatuwataki, hawa wote tunawarudisha na mpango wa kukagua shule zote ni endelevu,” amesema Haule.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted