Rais wa Afrika Kusini, Ramaphosa afanya mazungumzo na Rais wa Ukraine

Ramaphosa alitangaza kwamba alikuwa na mazungumzo ya simu na Zelensky “kujadili mzozo wa Ukraine na gharama yake pamoja na athari zake za kimataifa.”

0
Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye amekabiliwa na shutuma kali kwa kukataa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, siku ya Alhamisi alisema alikuwa amezungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Ramaphosa alitangaza kwenye Twitter kwamba alikuwa na mazungumzo ya simu na Zelensky “kujadili mzozo wa Ukraine na gharama yake ya kibinadamu, pamoja na athari zake za kimataifa.”

“Tunakubaliana juu ya haja ya kuwepo kwa mazungumzo ya kusitisha mzozo ambao umeathiri nafasi ya Ukraine kama muuzaji mkuu wa chakula katika bara letu,”alisema Ramaphosa.

Afrika Kusini, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, imedumisha msimamo wa kutofungamana na upande wowote tangu Urusi ilipoivamia Ukraine karibu miezi miwili iliyopita.

Licha ya hasira katika msimamo wake, Afŕika Kusini inasema kuwa mazungumzo ni chaguo bora kumaliza mzozo huo.

Nchi hiyo hadi sasa imejiepusha kupiga kura katika Umoja wa Mataifa dhidi ya Urusi.

Makumi ya mataifa mengine ya Kiafrika pia yamejizuia kupiga kura dhidi ya Urusi katika Umoja wa Mataifa.

Ramaphosa alisema Zelensky “anatarajia kuwepo kwa uhusiano wa karibu na Afrika katika siku zijazo.”

Zelensky ameomba kuhutubia Umoja wa Afrika, kwa mujibu wa mkuu wa sasa wa AU, Rais wa Senegal Macky Sall.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted