Mama amchoma mwanaye kwa maji ya moto kisa kula tambi bila ruhusa yake.

Chanzo cha tukio hilo ni mtoto huyo kuiba tambi ambazo ziliandaliwa kwa ajili ya chakula cha mchana, ndipo mama wa mtoto huyo alichukua hatua ya kumchoma kwa maji...

0
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, Shadrack Masija

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Kidinda Wilaya ya Bariadi, Mwamba Thomas (36) kwa tuhuma za kumuunguza kwa maji ya moto mtoto wake mwenye umri wa miaka minne akimtuhumu kuiba na kula chakula wakati alipokuwa matembezini.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Shadrack Masija amesema tukio hilo limetokea Aprili 22, 2022 ambapo amesema mtoto huyo alichomwa na maji ya moto kwenye mikono yake miwili na mama yake na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi kwa ajili ya matibabu.

“Chanzo cha tukio hilo ni mtoto huyo kuiba tambi ambazo ziliandaliwa kwa ajili ya chakula cha mchana, ndipo mama wa mtoto huyo alichukua hatua ya kumchoma kwa maji ya moto ambayo yalisababisha majeraha kwa mtoto,” amesema Masija.

Aidha mganga mfawidhi katika Hospitali ya Mji wa Bariadi Somanda, Yohana Costantine amesema wamempokea mtoto huyu akiwa na majeraha ya kuunguzwa na moto na amelazwa hospilini hapo kwa ajili ya matibabu.

“Tumempokea akiwa na majeraha makubwa mikono yote miwili, amelazwa hapa kwa ajili ya uangalizi na anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya Kwanza alivyoletwa hapa,” amesema Dk Costantine.

 Akiwa katika kitanda cha hospitali akiugulia maumivu mtoto huyo maarufu kwa jina na Hindia amesema alikula tambi akiwa na mdogo wake wakati ambao mama yao alipoondoka nyumbani na alivyorudi ndipo alimpiga pamoja na kumchoma maji ya moto mikononi.

“Alinipiga kisha akawasha moto na kuweka sufuria ya maji yalipochemka akaniweka mikono yote kwenye maji sufuria ikiwa jikoni,” amesema Hindia.

Mwamba Thomas anashikiliwa katika kituo Cha Polisi Bariadi na watoto wake wawili wakiwa chini ya uangalizi wa dawati la jinsia huku Hindia akiwa hospitali chini ya uangalizi wa maafisa wa ustawi wa jamii.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted