Sauti Sol yatishia kumshatki Odinga na muungano wa Azimio juu ya Hakimiliki ya Muziki

Sauti Sol ilikashifu muungano wa Azimio One Kenya Party inayoongozwa na Raila Odinga kwa kutumia wimbo wao “Extravaganza,” kwenye kampeini

0
Sauti Sol

Bendi ya muziki nchini Kenya Sauti Sol imetishia kumshtaki Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa madai ya ukiukaji wa hakimiliki katika kampeni zake za urais.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Mei 16, Sauti Sol ilikashifu muungano wa Azimio One Kenya Party inayoongozwa na Raila Odinga kwa kutumia mojawapo ya nyimbo zao, “Extravaganza,” kama wimbo wa kumtambulisha kiongozi wa Chama cha Narc Kenya Martha Karua kama mgombea mwenza wa muungano huo.

Sauti Sol imedai kuwa hatua iliyochukuliwa na timu ya kampeni ya Azimio ilikiuka haki yao ya kumiliki mali.

“Tumefahamishwa kuwa timu ya kampeni ya Azimio la Umoja imetumia moja ya nyimbo zetu asilia maarufu zaidi wimbo wetu “Extravaganza” bila leseni wala mamlaka, kama wimbo wa kutangaza wadhifa wa mgombea mwenza.”

Sauti Sol inaona kitendo hicho kama kinachokiuka haki zao za kimsingi za mali na uhuru wa kujumuika.

“Tumesikitishwa na Kampeni ya Azimio la Umoja ya kupuuza waziwazi haki yetu ya kudhibiti utumiaji wa hakimiliki yetu. Tutakuwa tunatafuta suluhisho la kisheria kwa ukiukaji huu wa wazi wa hakimiliki yetu,” bendi hiyo ilishikilia.

Akijibu madai hayo, Odinga kupitia chama chake – Orange Democratic Movement (ODM) – alidai kuwa kucheza wimbo huo ni onyesho la upendo kwa kikundi hicho cha muziki.

Wimbo wa Extravaganza ulitolewa mnamo 2019 ambapo kikundi kilishirikisha wasanii kadhaa akiwemo Nviiri, Bensoul, Crystal Asige, na Kaskazini.

Kauli yao inajiri siku chache baada ya Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya (MCSK) kuthibitisha kupokea Ksh562,500 kutoka kwa Raila kama ada ya leseni ya muziki kutumika katika kampeni zake, vyombo vya habari vya nchini vinaripoti.

Bodi ya Hakimiliki ya Kenya (KECOBO) ilitoa taarifa yake na kusema kuwa Azimio La Umoja One Kenya ilikosea ilipotumia wimbo wa Sauti Sol wakati wa kumtambulisha Martha Karua kama mgombea mwenza wa urais.

Bodi ilisema kwamba muungano wa Azimio ulihitaji kupata leseni ya upatanishi ambayo hutolewa tu na mtunzi na mchapishaji, katika kesi hii, Sauti Sol.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted