Waliojifanya maofisa wa Ikulu nchini Tanzania wakamatwa

Watuhumiwa hao ni Emmanuel John (38), mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam, Stanley George (34), mbeba mizigo na mkazi wa Temeke, Dar es Salaam pamoja na Mussa...

0

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kujifanya maofisa wa Ikulu, ambapo kwa kutumia kigezo hicho wamekuwa wakiwapigia simu na kuwatapeli viongozi mbalimbali wa serikali.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari ofisini kwake leo Juni 3,2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Henry Mwaibambe amethibitisha kukamatwa kwa watu hao.

Amewataja watuhumiwa kuwa ni Emmanuel John (38), mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam, Stanley George (34), mbeba mizigo na mkazi wa Temeke, Dar es Salaam pamoja na Mussa Nasoro (35) Dereva na Mkazi wa Mbagala Dar es Salaam.

“Katika upekuzi wamekutwa na simu nyingi na laini nyingi zenye majina ya viongozi wakubwa waandamizi wa serikalini.

“Aidha Emmanuel John yeye amekuwa akijitambulisha kama Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais. Watu hawa wamekuwa wakiwapigia na kuwasiliana na viongozi mbalimbali na kutoa sifa kuonesha kwamba Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu) anaridhishwa na utendaji wao wa kazi, kwa hiyo waendelee kuwasiliana,” ameeleza.

Kamanda huyo ameongeza kuwa: “Wengi tumewasiliana nao waliotapeliwa ni viongozi, wengine ni wakurugenzi wa halmashauri za miji, wengine ni viongozi wakubwa tu  wa serikali, wanawapigia wanawaambia tunatoka Ofisi ya Rais kwa hiyo tuwe karibu.”

Kamanda Mwaibambe ameeleza upelelezi wa watuhumiwa unaendelea kubaini mtandao mzima wa utapeli na pale utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zingine za kisheria.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted