Sudan: Maelfu ya kondoo wafa maji meli ilipozama

Meli hiyo ya mifugo ilikuwa ikisafirisha wanyama hao kutoka Sudan hadi Saudi Arabia ilipozama

0

Meli iliyojaa maelfu ya kondoo ilizama Jumapili katika bandari ya Suakin ya Red Sea nchini Sudan na kuwazamisha wanyama wengi waliokuwa kwenye meli hiyo lakini wafanyakazi wote walinusurika, maafisa walisema.

Meli hiyo ya mifugo ilikuwa ikisafirisha wanyama hao kutoka Sudan hadi Saudi Arabia ilipozama baada ya maelfu ya wanyama zaidi kupakiwa kuliko ilivyokusudiwa kubeba.

“Meli hiyo, Badr 1, ilizama Jumapili asubuhi,”afisa mkuu wa bandari ya Sudan alisema, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

“likuwa imebeba kondoo 15,800, ikiwa zaidi ya idadi inayostahili kubeba.” Afisa huyo alisema meli hiyo ilipaswa kubeba kondoo 9,000 pekee.

Afisa mwingine, ambaye alisema kuwa wafanyakazi wote waliokolewa, alitoa wasiwasi juu ya athari za kiuchumi na kimazingira za ajali hiyo.

“Meli iliyozama itaathiri utendakazi wa bandari,” afisa huyo alisema.

“Pia kuna uwezekano kuwa na athari za kimazingira kutokana na vifo vya idadi kubwa ya wanyama waliobebwa na meli.”

Omar al-Khalifa, mkuu wa chama cha kitaifa cha wasafirishaji bidhaa nje, alisema meli hiyo ilichukua saa kadhaa kuzama kwenye gati muda ambao lilimaanisha “ingeweza kuokolewa.”

Jumla ya thamani ya mifugo iliyopotea “ni karibu riyal milioni 14 za Saudia, sawa na dola milioni nne,” alisema Saleh Selim, mkuu wa kitengo cha mifugo cha jumuiya hiyo, akithibitisha pia kwamba kondoo hao walipakiwa kwenye meli kwenye bandari ya Suakin.

Alisema wamiliki wa mifugo walipata karibu kondoo 700 pekee lakini walipatikana wakiwa wagonjwa sana na hatutarajii waishi muda mrefu.”

Selim aliomba uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.

Mwezi uliopita, moto mkubwa ulizuka katika eneo la mizigo la bandari ya Suakin, uliodumu kwa saa kadhaa na kusababisha uharibifu mkubwa.

Haijabainika ni nini kilisababisha moto huo.

Uchunguzi umeanzishwa ili kubaini chanzo cha moto huo, lakini bado haijatoa matokeo yake.

Mji wa kihistoria wa bandari wa Suakin sio tena kitovu kikuu cha biashara ya nje ya Sudan, jukumu ambalo limechukuliwa na Port Sudan,ilioko kwenye pwani ya Bahari ya Shamu.

Kumekuwa na hatua za kuunda upya bandari ya Suakin, lakini mpango wa 2017 na Uturuki wa kurejesha majengo ya kihistoria na kupanua forodha ulisitishwa baada ya kuondolewa kwa rais wa muda mrefu Omar al-Bashir.

Sudan inasalia kukabiliwa na mzozo wa muda mrefu wa kiuchumi, ambao umeongezeka kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan.

Kupinduliwa kwa serikali kuliibua hatua kali, ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa misaada kutoka kwa serikali za Magharibi, ambazo zilitaka kurejeshwa kwa utawala wa mpito uliowekwa baada ya Bashir kupinduliwa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted