Tukio la mauaji ya Padri mkoani Mbeya lazua hofu kwa wananchi

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema tukio la mauaji ya kutisha ya Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Michael Samson (63) raia wa Malawi,...

0

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema tukio la mauaji ya kutisha ya Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Michael Samson (63) raia wa Malawi, limezua hofu miongoni mwa wananchi wa mkoa huo.

Kutokana na hali hiyo ameliagiza jeshi la polisi  kuongeza nguvu katika kufanya uchunguzi, ili kuwabaini wote waliohusika na mauaji ya padre huyo na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

 Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya, amewaambia  waandishi wa habari leo kuwa miongoni mwa watu ambao wamejawa na hofu kubwa kufuatia mauaji hayo ni pamoja na viongozi wa dini kutokana na chanzo cha tukio kutojulikana.

 Amesema awali mkoa ulikuwa umetulia ukiwa na amani ya kutosha, hivyo tukio hilo la ghafla limezua taharuki kwa wananchi jambo linaloleta umuhimu wa kutumia njia mbalimbali kulipatia majibu sahihi.

 Alisema jeshi la polisi linatakiwa kutumia njia mbalimbali kwenye uchunguzi wa tukio hilo, ili wahusika wapatikane na hatua zichukuliwe dhidi yao, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano pale jeshi litakapowahitaji kufanya hivyo.

“Kama serikali tunalaani vikali tukio hili, Mkoa wetu ulikuwa umetulia sana, lakini ghafla linatokea hili. Na kwa bahati mbaya sana tukio hili limetokea kwa mtumishi wa Mungu, tunaliagiza Jeshi la Polisi kutumia mbinu za kiintelijensia kuchunguza tukio hili kwa haraka sana,” alisisitiza Homera.

Aliwataka wananchi kutokatishwa tama na badala yake waendelee kuiamini serikali na Jeshi la Polisi na kwamba wahusika wa tukio hilo lazima watabainika na hatua kuchukuliwa.

 Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na kwamba uchunguzi utakapokamilika taarifa itatolewa, huku akisisitiza kuwa watazitumia taarifa zote watakazokuwa wanazipata kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

 “Sitaki kusema vitu ambavyo tumeanza kubaini kwa sababu jambo hili bado tunalichunguza, lakini niwahakikishie kwamba mpaka sasa tumeshaanza kupata baadhi ya taarifa na tutahakikisha tunafuatilia jambo hili mpaka mwisho,” alisema Kamanda Matei.

Aliwataka wananchi wa Jiji la Mbeya kutoogopa kupita katika eneo hilo, kwa maelezo kuwa usalama upo wa kutosha.

Kauli hiyo ya Kamanda Matei inaweza kuleta matumaini kwa kiasi na kuwaondolea hofu wananchi wa Kata ya Sisimba na maeneo ya jirani, ambao juzi walikubaliana kuacha kupita katika eneo la daraja la mto Meta eneo la Sabasaba hasa nyakati za usiku kutokana na tishio la mauaji ya Padri huyo.

Padri Michael aliyekuwa wa Shirika la wamisionari wa Afrika (White Fathers), mwili wake ulikutwa umetupwa chini ya daraja la Mto Meta lililopo Sabasaba jijini Mbeya ukiwa umeviringishwa kwenye blanketi na baadhi ya viungo vikiwa vimetenganishwa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted