Ukuaji wa Uchumi nchini Tanzania waongezeka

Hayo yamesemwa leo bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango nchini humo Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2021 na...

0
Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba.

Ukuaji wa uchumi wa Taifa la Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2021 umekuwa kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 mwaka 2020.

Hayo yamesemwa leo bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango nchini humo Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2021 na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2022.

Amesema kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi kumetokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO–19.

Amesema hatua nyingine ni uwekezaji wa kimkakati hususan katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.

“Shughuli za kiuchumi zilizokuwa na ukuaji mkubwa katika kipindi cha mwaka 2021 ni pamoja na sanaa na burudani (asilimia 19.4), umeme (asilimia 10.0), uchimbaji madini na mawe (asilimia 9.6) na habari na mawasiliano (asilimia 9.1)”

Aidha Waziri Mwigulu akizungumzia suala la mfumuko wa bei amesema umepanda kwa wastani  wa asilimia 3.7 kwa mwaka 2021 ukilinganisha na wastani wa asilimia 3.3 kwa mwaka 2020.

Amesema mfumuko wa bei umeendelea kuwa ndani ya lengo la wigo wa asilimia 3 hadi 5.

“Mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 Aprili 2022 ikilinganishwa na asilimia 3.3 Aprili 2021.

“Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kulichangiwa na sababu zilizo nje ya udhibiti wa serikali zikiwemo kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia kutokana na athari za vita baina ya Urusi na Ukraine,” Dk. Mwigulu.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted