Mabosi wa TPA wapandishwa kizimbani kwa kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 4.2

Waliofikishwa mahakamani kwa makosa hayo, ni Ofisa Rasilimali Watu wa mamlaka hiyo, Peter Gawile (58); Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi, Casmily Lujegi (65); Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi,...

0

Vigogo wanne wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania(TPA), wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matatu, likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 1.8 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 4.2. 

Waliofikishwa mahakamani kwa makosa hayo, ni Ofisa Rasilimali Watu wa mamlaka hiyo, Peter Gawile (58); Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi, Casmily Lujegi (65); Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Mashaka Kisanta (59) na Kilian Chale (51), ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Mshitakwa mwingine, Madeni Kipande, ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, hakuwepo mahakamani kusomewa mashitaka yake, kutokana na kufanyiwa upasuaji wa mgongo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI).

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Timotheo Mmari, jana Juni 30,2022, imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhan Rugemalira, kuwa kati ya tarehe 1 Oktoba 2014 na 1 Oktoba 2020, jijini Dar es Salaam, washitakiwa walikula njama na kuisababishia hasara TPA.

Aidha, kati ya tarehe 1 Januari 2015 hadi 17 Februari 2015, washitakiwa wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni Na. AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .

Vilevile, katika kipindi hicho cha 2014 na 2020, wakiwa huko TPA na maeneo mengine jijini Dar es Salaam, washitakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP), bila kupata kibali cha Bodi ya zabuni ya mamlaka.

Mbali na tuhuma hiyo, wote kwa pamoja, wanadaiwa kushindwa kufuata kanuni za zabuni na hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya Bodi, jambo lililosababisha TPA hasara hiyo.

Washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida kusikilizwa mahakama Kuu ama kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Upande wa mashitaka umeileza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo, bado haujakamilika na hivyo kesi imeahirishwa hadi 14 Julai mwaka huu.

Kwa upande mwingine, Hakimu Rugemalira alihoji upande wa mashitaka sababu za kuwaleta washitakiwa mahakamani wakati upelelezi hujakamilika, kwani watuhumiwa wanapaswa kufikishwa mahakamani wakati upelelezi ukiwa umekamilika, ili kuanza kusikiliza shauri husika na haki kutendeka.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted