Wajackoyah na Mgombea Mwenza watofautiana

Mgombea wa Roots Party, nchini Kenya Profesa George Wajackoya ametofautiana na mgombea mwenza Justina Wamae kufuatia madai ya kuidhisha mgombea Raila Odinga kuibuka

0
Mgombea wa chama cha Roots Profesa George Wajackoyah na mgombea mwenza Justina Wamae.

Zikiwa zimesalia siku tano kabla ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, chama ya Roots party kimeanza kukumbwa na dhoruba kali baada ya mgombea wa chama hicho Profesa George Wajackoyah kutofautiana na mgombea mwenza Justina Wamae kuhusu kuidhinisha mmoja wa wagombea wawili wakuu au kuendelea katika kinyang’anyiro hadi tamati.

Tofauti hiyo imetokea baada ya video kuibuka  mitandaoni ambapo Wajackoyah akiwa katika eneo la burudani mjini Kisumu ameonekana kumuunga mkono mgombea wa muungano wa Azimio One Kenya Raila Odinga.

“Niko hapa ili kujiunga na kundi la wana mapinduzi katika taifa hili.  Na kiongozi ninayemtazamia, mtu ambaye amefanya nisimame hapa si mwingine ila Raila Amollo Odinga.” Kinara huyo wa Roots  alisIkika akisema katika video hiyo.

Uongozi wa chama cha Roots hata hIvyo umejitokeza na kujitenga na madai hayo na kusema kuwa kanda hiyo iliitilafiwa ili kupigia debe mgombea fulani. Msemaji wa chama hicho  Jaymo Ule Msee, amesema Kinara wao alitoa heshima kwa wagombea  wote wa urais japo sehemu anayozungumza kumhusu Odinga ndio ilisIkika katika video hiyo. Msemaji huyo ameweka bayana kuwa chama hicho kiko imara na hakina mipango ya kujiondoa katika kipute cha kuelekea ikulu.

“Dhana kwamba profesa Wajackoyah amemuidhisha Raila Odinga ni potovu inayotumiwa na baadhi ya watu wanaotumika na mmoja wa wagombea wa urais.” alisema Ole Msee.

Hata hivyo mgombea mwenza wa Wajackoyah, Justina Wamae amepasua mbarika na kusema kuwa ni kweli Wajackoyah anamuunga mkono Raila Odinga. Wamae alisisitiza kuwa kamwe hakushauriwa kabla ya uamuzi huo kuchukuliwa na alisisitiza kuwa iwapo angeshauriwa angeunga mkono mgombea mbadala. “Ni kweli kusema mgombea na kinara wa chama anaunga mkono Azimio japo kama chama hatujakuwa na majadiliano kuhusu hatua hiyo. Na iwapo ningeshauriwa bila shaka ningekwenda kinyume.” alisema Justina Wamae.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted