Kenya: Je ni nani ataibuka mshindi?

Huenda wakenya wakafahamu kiongozi atakayechukua uongozi kutoka rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta leo

0
(COMBO/FILES) (Photo by Simon MAINA / AFP)

Huenda wakenya wakafahamu kiongozi atakayechukua uongozi kutoka rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta leo tarehe 15 Agosti, kwani tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC inaendelea kukamilisha zoezi la kujumuisha matokeo ya kutoka katika maeneo bunge yaliosalia.

Kufikia leo Jumatatu saa 4.45 tume ya IEBC ilikuwa imedhibitisha matokeo kutoka kwa maeneo bunge 248 kati ya maeneo bunge 291.

Hata hivyo, inakisiwa kuwa kuenda mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akatangaza matokeo hayo leo Jumatatu iwapo zoezi la kujumuisha matokeo hayo yatakamilika kwa wakati

Ikumbukwe kuwa Chebukati alisema kuwa atamtangaza mshindi katika uchaguzi wa urais mchana peupe.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, tume hiyo ina siku saba tangu siku wakenya walipoenda debeni kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo. Hiyo ina maana kuwa IEBC ina hadi kesho tarehe 16 Agosti kuwafahamisha wakenya ni nani kati ya naibu rais William Ruto na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga atakuwa anamrithi Kenyatta.

Katika Ukumbi wa Bomas of Kenya hali ya usalama umeimarishwa kufuatia utata ulioibuka usiku wa kuamkia tarehe 14 baada ya mawakala wa miungano ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja kuzozana kwa madai ya wizi wa kura.

Ingawa maafisa wa polisi wameongezwa katika lango la kuingia eneo la Bomas, walikuwa na wakati mgumu kuwaondoa baadhi ya waangalizi, viongozi wa mirengo tofauti na wafuasi wao milangoni na kuwazuia kutoingia katika ukumbi huo.

Gavana wa Kisumu-mteule Anyang’ Nyong’o, mwenzake wa Siaya James Orengo na Gavana wa Laikipia Ndiritu Murithi walizuliwa katika lango kuu la kuingia Bomas kwa muda.

Hali hiyo ilizua majibizano makali kati ya wafuasi wao na polisi. Hata hivyo baadaye waliruhusiwa kuingia ndani.

Mapema, katibu mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Veronicah Maina pia alizuiliwa kuingia Bomas hata hivyo baadaye alikubaliwa kuingia.

Hatua ya kuzua baadhi ya watu Bomas ni kati ya amri zilizotolewa na kamishna wa IEBC Abdi Guliye ambaye amekuwa akisisitiza kuwa ni mawakala wakuu wa wawaniaji wa urais, wasaidizi wao, makarani, wanadiplomasia, waangalizi na wanahabari tu ndiyo wanaoruhusiwa katika eneo hilo la kujumuisha matokeo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted