Ahukumiwa kunyongwa kwa kumuua mamamkwe

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Geita mwenye mamlaka ya ziada, Cleofas Waane, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.

0

Mahakama Kuu nchini Tanzania Kanda ya Mwanza imemhukumu mkazi wa Kaliua Mkoa wa Tabora, Gibe Masasila (40) kunyongwa mpaka kufa kwa kosa la kumuua mama mkwe wake Kabura Manyakenda.

Inadaiwa Masasila alimuua mkwewe huyo kwa kumcharanga mapanga kichwani, shingoni na mkononi na kufariki dunia papo hapo.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Geita mwenye mamlaka ya ziada, Cleofas Waane, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Waane alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama yake.

Alisema upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Winfrida Ernest, ulipeleka mahakamani mashahidi sita na vielelezo vitatu ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alimuua mama mkwe wake kwa kukusudia.

Pia alisema upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Kujitegemea Nestory Kuyula, haukuwa na shahidi yeyote zaidi ya mshtakiwa kujitetea peke yake.

Hakimu Waane alisema mshtakiwa alikuwa amemwoa Christina na walikuwa wakiishi Kaliua mkoani Tabora na Februari 15, 2018 mshtakiwa pamoja na mtu mmoja aitwaye Mateso walikwenda senta ya Kijiji cha Bwenda wilayani Bukombe kunywa pombe na ilipofika majira ya saa 2:00 usiku, walikwenda nyumbani kwao na mke wake aitwaye Christina.

Alisema walipofika, walimkuta mama mkwe wake Kabura Manyakenda akiwa anamuosha mjukuu wake na mkamwana wake aitwaye Pili Robert aliwapatia viti na wakakaa nje ya nyumba wakawa wanaota moto.

Hakimu alisema baada ya shahidi wa Jamhuri Pili Robert kuingia ndani ya nyumba hiyo, mtu mmoja aitwaye Mateso alimfungia Pili mlango kwa nje ndipo mshtakiwa Masasila alichukua panga na kuanza kumkatakata mama mkwe kichwani, shingoni na mkononi na kufariki dunia papo hapo.

Waane alisema wakati mshtakiwa  akimkatakata mapanga mama mkwe wake, shahidi Pili Robert alikuwa akimwona kwa kuchungulia kwenye dirisha ya nyumba hiyo kwa sababu ya mwanga kwa kuwa kulikuwa na moto nje pamoja na taa za Sola.

Alisema baada ya mshtakiwa huyo kusikia kelele kutoka kwa Pili Robert akiwa ndani ya nyumba na kuona mama mkwe wake kafariki dunia, alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Baada ya kitendo hicho, majirani walifika eneo la tukio na kumfungulia mlango Pili Robert na polisi pia walipofika ndipo Pili Robert aliwaambia kuwa mtu ambaye amemuua mama ni mume wa Christina anayeitwa Gibe Masasila.

Alisema polisi baada ya kupewa taarifa hizo, walimchukua mke wa mshtakiwa ambaye aliwapeleka polisi nyumbani kwa mshtakiwa Kaliua mkoani Tabora na kumkamata mshtakiwa huyo na kumfikisha kituo cha polisi Bukombe. Baada ya kufikishwa kituoni, mshtakiwa alihojiwa alikiri kumuua mama mkwe wake kwa sababu alimkataza mtoto wake Christina kuolewa na Masasila.

Hakimu Waane alisema chanzo cha kifo cha marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi, daktari alibaini kuwa ni kuvuja damu nyingi baada ya kupata majeraha makubwa sehemu za kichwani, shingoni na mkononi.

Waane alisema ameangalia ushahidi wa pande zote na kugundua kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote, hivyo kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kumuua mama mkwe wake kwa kukusudia.

Kabla ya kutolewa hukumu, Hakimu alimtaka mshtakiwa ajitetee ili kumpunguzia adhabu ndipo wakili wake Kuyula akaomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa madai kuwa amekaa muda mrefu gerezani pia ana familia inamtegemea.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Ernest, ulidai kuwa hauna kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa bali aiombe mahakama itowe adhabu kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Waane alitupilia mbali utetezi huo na kusema adhabu ya kesi ya mauaji ya kukusudia ni moja tu, hivyo mahakama inamhukumu mshtakiwa kunyongwa mpaka kufa na kama kuna upande ambao haujaridhika na hukumu hiyo, rufani iko wazi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted