Tanzania yaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa kuwarudisha wakimbizi wa Burundi nchini kwao

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nchini Tanzania,  Mhandisi Hamad Masauni amezitaka Jumuiya ya Kimataifa na Washirika wa Maendeleo kusaidia mchakato wa kuwarudisha Wakimbizi wa Burundi kwa...

0

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nchini Tanzania,  Mhandisi Hamad Masauni amezitaka Jumuiya ya Kimataifa na Washirika wa Maendeleo kusaidia mchakato wa kuwarudisha Wakimbizi wa Burundi kwa hiari nchini kwao kwa kuweka sawa mazingira ya ndani ya nchi hiyo.

Akizungumza katika kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR), alipokuwa anawasilisha taarifa ya Serikali katika Kikao hicho, jijini Geneva nchini Uswisi, Waziri Masauni amesema Serikali ya Burundi, Tanzania na UNHCR kupitia kikao cha Pande Tatu, walikubaliana ili kuwarejesha wakimbizi hao nchini kwao lazima hali ya mazingira ya ndani ya Burundi yaweze kuwa sawa.

Masauni ameongeza kuwa Burundi kwasasa ina amani na wakimbizi hao waliopo katika Kambi ya Nyarugusu na Nduta Mkoani Kigoma waweze kurudishwa kwao kwa hiari hivyo Jumuiya ya Kimataifa Washirika wa Maendeleo wanaweza kufanikisha mchakato huo kwa kuisaidia Burundi ili wakimbizi hao waweze kurudi katika nchi yao.

“Ili mpango huu ufanikiwe ni lazima hali ya mazingira ndani ya Burundi yaweze kuwa sawa, ili wakimbizi hao wanapoenda wasiweze kurudi nchini, kwahiyo tumewaomba shirika la kimaitaifa pamoja na washirika wa maendeleo kuisaidia Serikali ya Burundi kuhakikisha kwanza wanaweka mazingira mazuri kwa raia wa Burundi kurejea nchini kwao na kuendelea kubakia kule, na pia waendelea kusaidia huduma za wakimbizi katika nchi yetu,” alisema Masauni.

Aidha, Waziri Masauni alitoa pongezi kwa Kamishina Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi kwa kuteuliwa kwa mara nyingine katika nafasi hiyo katika kipindi kingine cha miaka miwili na nusu. 

Kikao hicho cha siku tano kilichoanza Oktoba 10, 2022 kinaendelea jijini Geneva ambapo wawakilishi kutoka nchi mbalimbali duniani wanaendelea kuwasilisha taarifa za wakimbizi na kujadiliwa na washiriki wa kikao hicho.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted