Hatimaye Makamishna Wanne wa IEBC wasimamishwa kazi rasmi.

Makamishna hao ni makamu mwenyekiti Juliana Whonge Cherera, makamishna Francis Mathenge Wanderi, Irene Cherop Masit na Justus Abonyo Nyang’aya

0
Makamishna wanne wa IEBC waliopinga matokeo ya urais agosti.

Rais William Ruto amewasimamisha kazi rasmi makamishna wanne wenye utata wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) na kubuni jopo la kuchunguza ombi la kuwaondoa afisini.

Katika notisi ya gazeti la serikali, ametoa agizo kuwa makamu mwenyekiti Juliana Whonge Cherera, makamishna Francis Mathenge Wanderi, Irene Cherop Masit na Justus Abonyo Nyang’aya waondoke afisini wakisubiri ushauri wa jopo hilo.

Rais Ruto amesema uamuzi huo umekuja kufuatia pendekezo la bunge lililotaka kuwaondoa makamishna hao kutokana na mienendo yao wakati wa uchaguzi mkuu wa agosti 9, 2022.

“Baada ya kupokea na kuzingatia ombi la bunge la kitaifa….mimi William Samoei Ruto, rais na kamanda mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Kenya, ninaagiza kwamba Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya, ambao ni makamishna wa tume ya IEBC, kusimamishwa kazi mara moja,” inasoma kipande cha notisi hiyo.

Rais ameendelea kuwateua jaji wa mahakama ya juu Aggrey Muchelule kuwa mwenyekiti wa jopo ambayo wanachama wake ni Carolyne Kamende Daudi, Linda Gakii Kiome, Mathew Njaramba Nyabena na Kanali Saeed Khamis Saeed.

Makatibu shirikishi wa mahakama hiyo watakuwa Kibet Kirui Emmanuel na Irene Tunta Nchoe huku Peter Munge Murage akiwa wakili mkuu na kusaidiwa na Zamzam Abdi abib.

Hatua ya rais Ruto inajiri siku moja baada ya bunge la kitaifa kuidhinisha ripoti ya kamati ya haki na masuala ya kisheria (JLAC) iliyopendekeza kuundwa kwa jopokazi ya kuchunguza mienendo ya makamishna hao wanne.

Mwenyekiti wa JLAC George Murugara alisema walikuwa na sababu za kutosha kuamuru kusimamishwa kazi kwa makamishna hao.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted