Rais Ruto akutana na viongozi wa Jubilee kabla ya mkutano wa Azimio katika uwanja wa Kamukunji

Hata hivyo, katibu mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni hakuwepo katika mkutano huo.

0
Rais William Ruto alipokutana na viongozi wa chama cha Jubilee mapema leo katika ikulu ya Nairobi.

Rais William Ruto ameandaa mkutano na wabunge wa zamani na wa sasa wa chama cha Jubilee kabla ya mkutano wa hadhara wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga katika uwanja wa Kamukunji.

Kulingana na Mbunge wa bunge la Afrika mashariki (EALA) Kanini Kega, mkutano huo ulilenga kujadili umoja wa eneo la Mlima Kenya na kukamilika kwa miradi ya maendeleo ambayo ilianzishwa na utawala uliopita.

Kanini amesema kama viongozi wa eneo la Mlima Kenya, walikuwa na  wasiwasi kuhusu miradi mingi ambayo serikali iliyopita ilikuwa imeanzisha ila wamebainisha kuwa serikali ya sasa ina nia ya kukamilisha miradi yote.

Mbunge huyo wa EALA amesema walichukua muda huo kusameheana na uongozi wa sasa kuhusu uhasama uliotokea wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana.

Hata hivyo, alibainisha kuwa bado wako katika Jubilee na upinzani ambao uko imara na pindi tu serikali ya Kenya Kwanza itakapokwenda visivyo watakuwa tayari kuikosoa vilivyo.

Lakini katibu mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni hakuwepo katika mkutano huo. Hivi majuzi Kioni alizungumzia udanganyifu ambao ulitekelezwa na tume ya uchaguzi IEBC aliodai ulimfanya rais Ruto kuwa mshindi katika uchaguzi huo.

Mkutano huo umefanyika kabla ya mkutano wa Azimio la Umoja One Kenya ambao utafanyika baadaye leo katika uwanja wa Kamukunji.

Wana Azimio wanalenga kutumia mkutano huo wa leo kujadili mambo yaliyofichuliwa hivi karibuni na kutoa taarifa kamili kuhusu yaliyojiri katika uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2022.

Viongozi wa Azimio wakiwemo Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Martha Karua, wiki jana waliahaidi kwamba kinara wao Raila Odinga atatoa taarifa kamili kuhusiana na ripoti inayoelezea jinsi uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulivyodaiwa kuibwa na kumpendelea rais Ruto.

Odinga mwenyewe amekuwa Afrika Kusini kwa wiki nzima kwa ajili ya misururu ya mikutano yake kama mwakilishi mkuu wa AU wa maendeleo ya miundombinu barani Afrika.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted