Rais Samia:Tuna dola za kututosha kutuhudumia miezi 4 tofauti na majirani zetu 

Rais Samia ametoa kauli hiyo jana Jumatano, katika mkutano wa hadhara wa Siku ya Wanawake Duniani ulioandaliwa na chama kikuu cha upinzani kupitia baraza lake la wanawake wa...

0

Rais wa Tanzania Samia Suluhu amewahakikishia wananchi kwamba nchi hiyo iko katika hali nzuri ya kiuchumi, tofauti na baadhi ya majirani zao katika ukanda wa Afrika Mashariki 

Rais Samia ametoa kauli hiyo jana Jumatano, katika mkutano wa hadhara wa Siku ya Wanawake Duniani ulioandaliwa na chama kikuu cha upinzani kupitia baraza lake la wanawake wa CHADEMA, alisema nchi hiyo iko imara kiuchumi kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika Mashariki.

“Ndugu zangu nataka niwaambie kuwa Tanzania iko vizuri kiuchumi. Katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki, sisi ni bora kuliko nchi nyingine, mtu asikudanganye. Sasa hivi kila nchi inalalamikia uhaba wa dola ilhali tunazo za kutufikisha miezi minne,” alisema Samia

Alisema Tanzania imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa majirani wanaokabiliana na uhaba wa dola ili kudhamini uagizaji wao wa mafuta ghafi kutoka nje ya nchi.

“Nendeni kwa majirani zetu, hawana hata bidhaa ya wiki mbili. Tunapokea maombi ya kudhamini ugavi wao wa mafuta lakini tumekuwa tu tukijifanya kuwa hali ni mbaya kwetu pia, ” alisema na kuongeza kuwa 

“Tunafanya vizuri na uchumi wetu utakuwa na nguvu zaidi ikiwa tutaendelea kuwa na umoja.”

Kauli ya Samia imekuja wakati ambapo taarifa zinaitaja nchi ya Kenya kuwa ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa dola za Marekani kwa sasa, ambao umechangiwa na shinikizo la ulipaji wa deni la nje.

Taarifa hizo zinaeleza pia Mahitaji ya fedha za kigeni yameongezeka hivi karibuni huku waagizaji wakitafuta dola zaidi kutokana na ongezeko la bei za kimataifa za mafuta, bidhaa za chakula, mafuta ya kupikia na chuma, miongoni mwa mengine.

Kwa mujibu wa takwimu iliyotolewa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) wiki iliyopita inaonyesha akiba ya fedha za kigeni ilishuka hadi $6.6 bilioni (Ksh.845.46 bilioni) mnamo Machi 2 kutoka $6.86 bilioni (Ksh.878.76 bilioni) mnamo Februari 23.

Na wakati Gavana wa CBK Patrick Njoroge amepuuza uhaba huo kila mara, hii ni miezi 3.69 ya malipo ya uagizaji bidhaa, ambayo ni chini ya kiwango cha miezi minne kilichowekwa.

Kuna hofu ya kuzuka kwa uhaba wa mafuta nchini kote na madereva wiki hii wamekataliwa kutoka kwa vituo maalum vya kujaza mafuta.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa  tatizo hilo lilitokana na uhaba wa dola na kusababisha maduka hayo kushindwa kununua bidhaa za mafuta.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted