Kimbunga Freddy: Rais wa Malawi atangaza maombolezo ya kitaifa ya siku 14

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza siku kumi na nne za maombolezo ya kitaifa baada ya zaidi ya watu mia mbili ishirini kufariki dunia

0

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza siku kumi na nne za maombolezo ya kitaifa baada ya zaidi ya watu mia mbili ishirini kufariki dunia katika mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na kimbunga Freddy.

Rais Chakwera ameomba msaada wa kimataifa kusaidia katika shughuli za uokozi na kulijenga upya taifa hilo baada ya mvua kubwa iliyonyesha kwa siku sita kusababisha maafa makubwa nchini humo.

“Malawi iko katika hali ya janga,kile kimbunga Freddy imefanya ni kuturudisha nyuma ilhali tulikuwa tunajijenga upya kutokana na majanga ya kipindi cha nyuma.Naiomba jumuiya ya kimataifa kutuangalia kwa jicho la huruma kwasababu tunahitaji msaada,tunahitaji msaada wa kuwashughulikia manusura ambao wamepoteza kila kitu.Wanahitaji vitu vya msingi,makazi,mavazi,chakula.”

Mamlaka inasema takriban watu 41 bado hawajulikani walipo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo kusomba nyumba zao.

Zaidi ya 4000 wameyahama makazi yao na kwa sasa wanahifadhiwa katika majengo ya muda kote nchini.

Rais pia alisema mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri uliidhinisha kutolewa kwa dola milioni 1.5 kusaidia maelfu ya Wamalawi walioathiriwa na dhoruba.

Rais Chakwera alisema fedha hizo hazitatosha.

“Hali ya uharibifu tunayokabiliana nayo hapa ni kubwa kuliko rasilimali tulizonazo.”

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted