Simbachawene atetea hoja kuhusu kinga kwa maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema kinga inayokusudiwa kuwekwa kwa maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa...

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema kinga inayokusudiwa kuwekwa kwa maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa itatumika tu endapo walikuwa wakitekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa kwenye sheria.

Akihitimisha hoja bungeni jijini Dodoma kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa wa Mwaka 2023, amesema endapo afisa wa idara hiyo atatenda kosa nje ya majukumu yake yaliyoanishwa kisheria, basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Tunazungumzia kinga katika kulinda usalama wa nchi,” amesema 

Simbachawene huku akisisitiza kuwa jukumu la chombo hicho si tu kulinda nchi dhidi ya vitisho vya ndani, bali pia kinalinda usalama dhidi ya maadui wa nje na mipango ya nchi ya maendeleo.

Amesema watu wanaopinga au kuwa na wasiwasi ikiwemo katika mitandao ya kijamii, ni kwa sababu hawajapitia mambo mazuri yaliyofanyika kwenye Muswada huo, na kwamba wakisoma wataelewa kwani hakuna chochote chenye nia mbaya kilichofanyika.

“Msingi mkubwa ni amani, mshikamano na amani ya nchi yetu na kulinda nchi yetu kama jukumu la kila Mtanzania na wenzetu hawa wamepewa jukumu hilo hivyo lazima tuwakinge dhidi ya mambo fulani fulani wanayoweza kuwa wanatekeleza,” amesema Waziri Simbachawene

Baada ya mjadala huo, Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa wa Mwaka 2023 na sasa utakwenda kwa Rais kwa ajili ya kusainiwa kuwa sheria, lengo likiwa ni kuboresha ufanisi wa idara hiyo kuendana na mahitaji ya sasa ya uongozi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted