BMH yapandikiza uume kwa mara ya kwanza nchini Tanzania

Kiongozi wa chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo (TAUS) Dk Lyuba Nyamsogoro amesema kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na uwepo wa watu wengi wenye...

0

Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) iliyopo nchini Tanzania jijini Dodoma kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa  wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo nchini humo (TAUS) pamoja na daktari bingwa kutoka nchini Ufaransa kwa mara ya kwanza,Juni 14, 2023 imefanikisha upasuaji wa kupandikiza uume kwa watu wawili waliokuwa na matatizo ya nguvu za kiume.

Upasuaji huo uliofanywa na jopo hilo ni kwa wale wanaume ambao uume wao umeshindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa mbalimbali.

Akizungumza baada ya kukamilisha upasuaji huo daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Remigius Rugakingira amesema upasuaji huo umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.

“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasuaji wa aina hii kilichofanyika hapa ni kuweka vipandikizi maalumu vitakavyo wezesha uume kurudi katika hali yake ya awali.

“Upasuaji huu tumeshirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo pamoja na daktari bingwa wa mfumo wa mkojo kutoka Ufaransa na tumefanikiwa katika hilo,” amesema Dk Rugakingira.

Amesema kuwa huu ni wito kwamba Hospitali ya Benjamin Mkapa inajali afya ya wanaume na upasuaji kama huu unaweza kufanyika Tanzania.

Kiongozi wa chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo (TAUS) Dk Lyuba Nyamsogoro amesema kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na uwepo wa watu wengi wenye matatizo ya nguvu za kiume nchini na Afrika kwa ujumla.

“Moja wapo ya dhumuni ya TAUS ni kuendeleza wataalam nchini kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ili kuleta teknolojia inayopatikana duniani nchini Tanzania na kutibu magonjwa kama haya kwa wale wenye matatizo,” amesema Dk Nyamsogoro.

Msemaji wa BMH Jeremiah Mbwambo ameeleza, “Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume, Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuiwezesha teknolojia za kisasa za matibabu ili kuwapatia matibabu thabiti wananchi,” amesema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted