Watu wawili wafa maji mkoani Pwani

Matukio ya vifo hivyo yametokea kwa nyakati tofauti ikiwa ni sehemu ya madhara kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

0

Watu wawili wamefariki mkoani Pwani mmoja kwa kusombwa na maji na mwingine kuzama wakati akiogelea.

Matukio ya vifo hivyo yametokea kwa nyakati tofauti ikiwa ni sehemu ya madhara kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutuma amesema miongoni mwa waliofariki, ni pamoja na mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi  Chambasi, wilaya ya Kisarawe, ambaye kifo chake kimetokea wakati akiogelea jirani na makazi yao.

“Huyu mwanafunzi alifariki baada ya kuzama dimbwi lililokuwa limejaa maji jirani na nyumbani kwao,” amesema kamanda huyo, huku akimtaja Ally Haji ambaye alifariki baada ya kusombwa na maji wakati wakati akijaribu kuvuka mto huko Mindukeni Chalinze mkoani Pwani.

“Alikuwa navuka kwenye mto uliopo maeneo ya Mindukeni lakini kwa bahati mbaya akasombwa na maji na mwili wake ukaokotwa na baadaye kupewa familia kwaajili ya shughuli za maziko,” amesema.

Kwa mujibu wa Kamanda hyo, matukio ya vifo hivyo yalitokea Novemba 13, 2023; ambapo ametoa tahadhari kwa wananchi mkoani humo kuchukua tahadhari ya mvua kwa kipindi hiki ili kulinda usalama wao na mali zao.

Amesema kuwa jeshi hilo limeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari kipindi hiki mvua zinapoendelea kunyesha na kusisitiza kuwa wanapaswa kuzingatia hilo ili kulinda familia ikiwemo wanafunzi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted