Ushuhuda Mjamzito Kujifungulia Njiani, Kisa Ubovu Wa Barabara Ya Mbeya – Njombe

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza ameendelea na ziara yake katika kata ya Ilungu akikutana na wananchi wake na kuendelea kusikiliza kero zinazowakabili kwa ajili ya Serikali kuzitafutia ufumbuzi.

Akiwa huko amekutana na wananchi wa vijiji vya Mwela, Shango na Kikondo ambapo wameshukuru kwa utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo umeme vijijini.

Pamoja na pongezi zao kwa Serikali, wameeleza kilio chao kikubwa kwa wakazi wa Kikondo kuwa ni ubovu wa barabara ya Isyonje Kikondo yenye urefu wa kilomita 22, uhitaji wa kituo cha afya kwa wananchi wa vijiji vya Mwela, Shango na Kikondo pamoja na uhitaji wa nishati ya umeme kwenye vitongoji kwa maeneo ambayo bado haujafika.

Katika kata hiyo wananchi wamesema barabara zimekuwa mbovu hasa msimu wa mvua kiasi cha kuwafanya baadhi ya wanawake kujifungulia njiani wakati wakienda kutafuta huduma za kiafya.

Wameitaka Serikali kuboresha barabara hiyo kuwa ya lami kama ambavyo imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa muda mrefu ili pia kuwasaidia kwenye shughuli za usafirishaji mazao.

Akijibia kero hiyo Kaimu meneja wa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya Mhandisi Kamokene Sanke, amesema “Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Isyonje Kikondo tumeongeza nguvu kwa kuweka wakandarasi wawili na wiki ijayo tutakuja kumwonyesha mkandarasi site kwasababu huku hakufahamu baada ya hapo mitambo itaanza kuletwa ili kazi ianze”, ameeleza Mhandisi Sanke.

Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza ameahidi kutowaangusha wananchi wake kwa kuhakikisha kero zao zinaendelea kutafutiwa mwarobaini hasa za umeme pamoja na miundombinu ya barabara.

Mbunge Njeza amesema kutokana na maelezo hayo ya Serikali ni imani yake kuwa barabara hiyo itaanza kujengwa hivi karibuni kwa kiwango cha lami kwakuwa tayari ilishaombewa bajeti na tatizo lilikuwa awali kwa mkandarasi wa kwanza hivyo kuwaomba wananchi wake kuendelea kuwa wavumilivu akisema miundombinu ya barabara itaendelea kurekebishwa ili ipitike kwa urahisi nyakati zote.

TAARIFA NA JOSEA SINKALA, MBEYA