Meya wa Ufilipino awaamuru wafanyikazi wa umma ‘watabasamu’ au watozwe faini

Meya wa Ufilipino amewaamuru watumishi wa umma kutabasamu, au huenda wakatozwa faini, huku akijaribu kuboresha kiwango cha huduma zinazotolewa na serikali ya eneo hilo.

Aristotle Aguirre alianzisha ‘sera ya tabasamu’ mwezi huu baada ya kuapishwa kuwa meya katika mji wa Mulanay katika jimbo la Quezon, kwenye kisiwa kikuu cha Luzon.

Sera hiyo lazima ipitishwe ‘wakati wa kuwahudumia watu ili kutoa huduma bora na kuonyesha hali ya utulivu na hali ya kirafiki” amri ya utendaji ilisema.

Aguirre alisema hatua hiyo ni kutokana na malalamiko kutoka kwa wenyeji, wengi wao wakiwa wakulima wa nazi na wavuvi, kuhusu unyanyasaji ambao wanapata kutoka kwa wafanyakazi wa ofisi za serikali walipoenda kulipa kodi au kutafuta huduma.

Baadhi ya raia hutembea kwa muda wa saa moja kutoka vijiji vyao vya mbali ili kufikia ukumbi wa jiji.

“Wanapofika, wanasikitishwa na tabia ya watu wanaofaa kuwahudumia nao,” Aguirre alisema.

Aguirre, ambaye alikuwa mtaalamu wa masuala ya kazi kabla ya kuwania wadhifa huo katika uchaguzi wa Mei 9, anataka ‘kubadilisha mtazamo wa wafanyikazi wetu wa serikali.’

“Tunahitaji kuwa manispaa yenye kupokea wateja kwa urafiki na tabasamu,” alisema Aguirre, mwanawe katibu wa zamani wa sheria katika utawala wa rais wa zamani Rodrigo Duterte.

Wafanyakazi ambao hawatatii agizo hilo wanaweza kutozwa faini inayolingana na mshahara wa miezi sita au kusimamishwa kazi.

Alipoulizwa jinsi sheria hiyo itatekelezwa wakati Wafilipino bado wanahitajika kuvaa barakoa hadharani, Aguirre alisema watu wanaweza kuhisi ikiwa kuna mtu anawasaidia kwa dhati.

“Sidhani kama tutafikia hatua hiyo,” Aguirre alisema kuhusu adhabu zinazoweza kuwakabili.

“Unahitaji kuwa na vibes nzuri kwa wafanyikazi wetu na raia.”