Simba sita waliuliwa baada ya kutoroka kutoka kwa mbuga ya wanyama ya Afrika Kusini na kuwatia hofu watu wanaoishi karibu, mamlaka ya wanyamapori ilisema Jumatatu.
Walinzi katika jimbo la mashariki la KwaZulu-Natal waliwaua simba hao siku ya Ijumaa baada ya wakaazi kuandamana kuwa hawawezi tena kutembea kwa usalama usiku, mamlaka ilisema.
“Hasira ilikuwa ikiongezeka huku ikihofiwa kuwa simba hao walikuwa hawaogopi binadamu tena,” msemaji wa Ezemvelo KZN Wildlife Musa Mntambo alisema katika taarifa yake.
Simba walikuwa wameua takriban ng’ombe sita na hawakukimbia tena walipokutana na wanadamu na badala yake walitembea kuelekea kwao, alisema.
Ulimwenguni kote idadi ya simba wanaoishi porini inapungua, lakini idadi ya wanyama hao nchini Afrika Kusini inazidi kuongezeka, kuna takriban simba 3,500 karibu mmoja kati ya sita ya jumla ya dunia, kulingana na mashirika ya wanyamapori.
Mntambo alisema wakazi wa eneo hilo ‘wamekuwa wakiishi kwa hofu,” na kuongeza kuwa baadhi hawatajiingiza tena katika maeneo yanayotumika kama malisho ya mifugo yao.
Mapema mwezi huu baadhi ya wananchi walikata uzio wa pembezoni mwa mbuga ya Hluhluwe ambapo simba walitumia kutoroka.
Mntambo alisema simba hao wamekuwa wakitumia matundu kwenye uzio karibu na mikondo ya maji kutoroka kutoka kwa hifadhi hiyo.
Mnamo mwaka wa 2016, mfanyakazi katika hifadhi hiyo aliuawa na simba jike.