Polisi wa Malawi wawakamata watu 76 baada ya maandamano ya siku nzima

Polisi katika mji mkuu wa Malawi Lilongwe walisema iliwakamata watu 76 Jumatano baada ya maandamano dhidi ya kasi ndogo ya mahakama katika kushughulikia kesi za ufisadi na kupanda kwa gharama ya maisha.

Msemaji wa polisi wa Lilongwe, Hastings Chigalu ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wamewakamata viongozi wanane wa waandamanaji ambao watafunguliwa mashtaka ya kukusanyika kinyume cha sheria na kudharau mahakama.

“Watu wengine watafunguliwa mashtaka ya wizi na kusababisha fujo kwa umma,” alisema.

Chigalu alidai kuwa wahalifu waliojipenyeza kwenye maandamano walipora maduka ya raia wa kigeni katika vitongoji kadhaa vya jiji hilo.

Polisi na waandamanaji walikabiliana katika vitongoji vya Area 36, ​​Area 23 na Falls Estate baada ya waandamanaji kufunga barabara kuu kwa matairi ya moto.

“Ndio maana polisi walifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji, ambao waliingia mijini na kuanza kupora maduka,” alisema mkazi wa Falls Estate Matt Chimseu.