Kenya imerejelea mauzo ya mirungi hadi Somalia siku ya Jumapili, wiki moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kukubaliana kuhusu kufunguliwa tena kwa mpaka kati ya nchi hizo mbili ili kurahisisha usafiri wa watu na kuimarisha biashara ya bidhaa na huduma.
Waziri wa Kilimo wa Kenya Peter Munya alithibitisha kuondoka kwa ndege kutoka Nairobi iliyobeba shehena ya miraa.
“Ndege ya mizigo ya miraa iliondoka Nairobi kuelekea Mogadishu leo asubuhi,” Waziri wa Kilimo Peter Munya alisema.
Mwakilishi wa wafanyabiashara wa mirungi nchini Kenya alithibitisha kusafirishwa kwa shehena hiyo.
“Ni kweli kwamba shehena ya kwanza ya ndege ya mizigo iliondoka leo asubuhi. Hata hivyo, tunatoa wito wa mawasiliano rasmi kutoka kwa mamlaka ya Somalia kuhusu kuanzishwa tena kwa usafirishaji wa miraa,” alisema Kimathi Munjuri, mwenyekiti wa Nyambene Miraa Trade Association.
Somalia ilitangaza kupiga marufuku mirungi kutoka Kenya mnamo Machi 2020 huku kukiwa na mzozo wa mpaka wa baharini kati ya majirani hao wawili wa Afrika Mashariki.