Marekani imetangaza kuwa ujumbe wa rais Joe Biden utahudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mteule wa Kenya William Ruto siku ya Jumanne, tarehe 13 mwezi huu wa Septemba.
Katika taarifa kutoka ikulu ya Whitehouse, rais wa Marekani Joe Biden amethibitisha kuwa ujumbe wa watu watano utakaoongozwa na mwakilishi wa kibiashara wa Marekani Katherine Tai utakuwepo katika hafla hiyo kuwakilisha Marekani .
Wajumbe wengine ni pamoja na Balozi wa Marekani nchini Kenya Mheshimiwa Meg Whitman, mwakilishi wa Marekani kutoka Texas Colin Allred, Katibu Msaidizi wa ofisi ya masuala ya Afrika Mary Catherine Phee, msimamizi msaidizi wa ofisi ya Afrika wa shirika la maendeleo ya kimataifa ya Marekani Dk. Monde Muyangwa.
Matayarisho kwa ajili ya siku hiyo ya kihistoria yamekamilika huku jukwaa ikiwa imetengenezwa na maafisa wa vikosi tofauti vya kijeshi ukiendelea na mazoezi kwa ajili ya siku hiyo.
Katibu wa kudumu katika wizara ya usalama wa ndani Karanja Kibicho amebaini kuwa wanatarajia wakuu wa mataifa takribana 20 kutoka bara la Afrika.
Pamoja na hao wageni mashuhuri 2,500 watakuwepo katika wakati wa hafla hiyo. Kibicho ambaye ni mwanachama wa kamati ya mpito amedokeza kuwa wizara ya nchi za kigeni imefanya mipango ya kuwapokea na kuwahifadhi wageni hao.
“Itifaki zote zinazohusiana na wakuu wa nchi za kigeni wanaokuja wizara ya mambo ya Nje tayari imefanya mipango kuhusu jinsi watapokelewa na kuandaliwa malazi na usafiri” alisema Kibicho.
Kibicho amesema wanatarajia kuwa uwanja wa Kasarani ambayo ujazwa na watu 60,000 kujazwa hadi pomoni na amewataka wakenya ambao wanapanga kuhudhuria kufika na kuketi kabla ya moja asubuhi.
Kwa watakaochelewa na kupata uwanja umejaa televisheni zimeandaliwa nje ya uwanja ili wawezi kufuatia kitakachokuwa kinaendelea ndani ya uwanja huo.
Milango ya uwanja yatafunguliwa saa kumi asubuhi kwa watakaohitaji kufika na kuketi mapema.
Wizara ya usalama wa ndani imewahakikishia wote wanapania kufika uwanjani humo kuwa kutakuwepo usalama wa kutosha.
Maafisa 10,000 wa polisi wamewekwa katika uwanja huo kuhakikisha kuna usalama wa kutosha na mambo yanakwenda kulingana na ratba.
Wakati huohuo, Kibicho ametoa hakikisho kuwa kila kitu ki shwari kwa ajili ya siku hiyo na kwamba kamati ya mpito imeridhishwa na maandalizi hayo.
Rais mteule William Ruto atachukua hatamu za uongozi rasmi kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta ambaye amekuwa mkubwa wake kwa miaka 10 iliyopita.