Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na kutumikia kifungo cha muda mfupi gerezani, amesema yuko tayari kwa kurudishwa kisiasa na chama tawala.
Katika taarifa yake Jumatatu jioni, Zuma mwenye umri wa miaka 80, alisema ameombwa na wanachama wa chama cha African National Congress (ANC), ambacho kimeitawala Afrika Kusini tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, kujiweka mbele wakati chama hicho kikijiandaa kuchagua uongozi mpya.
“Sitakataa wito kama huo iwapo wataona kuna umuhimu kwangu kulitumikia shirika hilo tena,” alisema, akiongeza kuwa amekuwa akishauriana na viongozi wa chama “licha ya matatizo yaliyosababishwa na hali yangu ya sasa ya kisheria”.
Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na mapigano makali ndani ya ANC, kabla ya mkutano wa kitaifa wa uchaguzi mwezi Disemba.
Chama hicho kinatarajiwa kufanya uchaguzi wa ndani ili kumchagua kiongozi mpya, ambaye baadaye atakuwa mgombea wa uchaguzi ujao wa urais mwaka 2024.
Rais wa sasa Cyril Ramaphosa ana matumaini ya kupata muhula wa pili lakini anakabiliwa na changamoto kutoka kwa kundi linalomtii Zuma – mtu wa mgawanyiko ambaye jina lake linahusisha na rushwa kwa waafrika Kusini wengi lakini bado ni shujaa kwa wanachama wengi wa mashinani wa ANC.
Zuma amesema anamuunga mkono mke wake wa zamani Nkosazana Dlamini-Zuma kuchukua nafasi ya Ramaphosa na kudokeza kuwa atakuwa tayari kuhudumu kama mwenyekiti wa chama, jukumu jingine muhimu.
Uungwaji mkono kwa chama cha Nelson Mandela ulishuka chini ya asilimia 50 kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, na serikali inakabiliwa na hali ya kutoridhishwa na umaskini ulioenea, ukosefu wa ajira, na mgogoro wa muda mrefu wa umeme.
Zuma akawa rais mwaka 2009 lakini akalazimika kuachia madaraka miaka tisa baadaye ili kumpendelea Ramaphosa, aliyekuwa makamu wa rais.
Julai mwaka jana alifungwa jela miezi 15 kwa kosa la kudharau mahakama baada ya kukataa kutoa ushahidi kabla ya uchunguzi wa rushwa lakini akaachiliwa kwa msamaha wa matibabu miezi miwili tu katika muhula huo.