Mwanasiasa Sam Matekane siku ya Ijumaa alikula kiapo cha kuwa waziri mkuu mpya wa Lesotho katika uwanja wa Setsoto uliofurika katika mji mkuu, Maseru.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 64, ambaye aliwasili katika sherehe ya kuapishwa kwake akiwa ndani ya gari aina ya Rolls Royce, aliapa kurejesha matumizi ya serikali pamoja na kuchapisha ukaguzi wa mtindo wa maisha yeye mwenyewe na mawaziri wake wanaoingia madarakani.
“Serikali ya Lesotho inaapa kwamba itakuwa wazi kwa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni,” Waziri Mkuu mpya alisema katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa siku ya Ijumaa.
Alianza kwa kuwashukuru watu wa Lesotho na kusema anakubali kirungu hicho ili kuifanya Lesotho kuwa bora tena.
Matekane, ambaye ataongoza moja ya nchi maskini zaidi duniani, alisema atachukua vipande vya nchi ambayo imekuwa katika mdororo wa uchumi tangu mwaka 2017.
Matekane amesema kutokuwa na uwezo kwa sekta binafsi kutimiza wajibu wake katika kutengeneza ajira, kumeathiri sekta ya umma.
“Hata hivyo… sekta ya umma yenyewe haina mapato ya kutegemewa, hali ambayo huenda ikawa mbaya Zaidi,” aliongezea.
Katika mahojiano na vyombo vya habari kabla ya uchaguzi, Matekane alisema anatarajia kugeuza mambo, kuleta ujuzi wake wa kibiashara kwa serikali ili kufufua uchumi na kukabiliana na madeni ya umma na ukosefu wa ajira.
Maelfu ya raia wakijikinga na miavuli ya rangi ili kuepuka jua kali walimkaribisha waziri mkuu wao mpya wakiimba nyimbo na kupuliza pembe – maarufu kama vuvuzela katika nchi jirani ya Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa Revolution for Prosperity (RFP) anakuwa waziri mkuu wa kumi wa Lesotho baada ya chama chake kushinda viti 56 vya ubunge kati ya 120 baada ya uchaguzi wa Oktoba 7, miezi sita tu baada ya kuanzishwa kwake.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye nchi yake inaizunguka kabisa Lesotho, alikuwa mmoja wa viongozi wa kikanda waliohudhuria sherehe hizo.
“Dhamana imara ya mataifa yetu mawili imejengwa juu ya uhusiano wa familia, lugha ya pamoja, historia… zamani zetu hazitenganishwi na mustakabali wetu pia unaingiliana” Ramaphosa alisema katika hotuba yake ya pongezi.
Rais wa Marekani Joe Biden pia alituma ujumbe kwenye sherehe hizo.
Lesotho, yenye idadi ya watu milioni 2.2, inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, huku zaidi ya asilimia 30 ya wakazi wake wakiishi chini ya dola 1.90 kwa siku.