Mwanamme wa makamo wa taifa la Nigeria, ambaye ni mlanguzi sugu wa dawa za kulevya ameshtakiwa kwa kosa la kuingiza gramu 647.7 za heroini nchini Kenya zenye thamani ya shilingi za Kenya1.9 kutoka Tanzania.
Kulingana na mwendesha mashtaka, tarehe 4 julai mwaka wa 2018 katika afisi za usafirishaji za kampuni ya basi la Tahmeed mjini Dares salaam Martin Ike aliyeandamana na jamaa mwingine walisafirisha kuelekea Kenya heroin kinyume cha sheria za dawa za kulevya kipengee cha 4 ya mwaka 1994.
Ripoti za maafisa wa polisi zinaonyesha Martin Ike alikamtwa nchini Nigeria na maafisa wa kitengo cha polisi wa Interpol na kusafirishwa hadi Kenya ambapo alikabidhiwa kwa mamlaka kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa iliyosomwa mbele ya jaji wa mahakama hiyo, ilisema Ike amekuwa mafichoni tangu polisi nchini Kenya walipotangaza kwamba alikuwa mhalifu anayesakwa zaidi kwa kusafirishwa dawa za kulevya aina ya heroin.
Mshukiwa huyo ambaye alifikishwa mbele ya hakimu mkaazi mkuu wa Mombasa Vincent Adet alikana shtaka hilo la ulanguzi wa dawa za kulevya.
Hakimu huyo ameamuru mshukiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Bandari, akisubiri kuskizwa kwa ombi lake la dhamana kesho tarehe 12 januari mwaka huu.
Hata hivyo, mkurugenzi wa mashtaka ya umma amepinga kuachiliwa kwa mshukiwa huyo kwa misingi kuwa ni mlanguzi wa dawa za kulevya aliyetoroka bila pasipoti halali.
Pamoja na hayo, mkurugenzi huyo wa mashataka amesema tangu polisi watangazea kuwa yeye ndiye mhalifu sugu wa ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroin, Ike amekuwa akichezea maafisa wa polisi mchezo wa paka na panya kutoka nchi moja hadi nyingine.
Katika utetezi wake, wakili wa Ike Geoffrey Were alipinga taarifa ya DCI akisema mteja wake hakuwa mtoro bali amekuwa gerezani nchini Tanzania kwa miaka mitano.
“Mweshimiwa, mshtakiwa aliyefikishwa mbele ya mahakama alirudi kutoka katika gereza la Dares salaam rumande ya Keko na amekuwa akizuiliwa katika gereza hilo tangu mwaka wa 2018 hadi sasa.” wakila wa mshtakiwa aliiambia mahakama.