Idadi ya waliofariki katika ajali ya barabarani nchini Kenya imeongezeka hadi 52, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alisema Jumamosi.
Kisa hicho kilitokea Ijumaa jioni katika mji wa Londiani katika kaunti ya Kericho magharibi.
Polisi walisema kuwa ajali hiyo ambayo ni moja ya vifo vingi zaidi nchini Kenya kwa miaka kadhaa, ilitokea wakati lori lilipopoteza mwelekeo na kuyagonga magari mengine kadhaa na watembea kwa miguu kwenye makutano yenye shughuli nyingi.
Hadi sasa miili thelathini na saba kati ya watu 52 walioangamia katika ajali hiyo imetambuliwa.
Msimamizi wa Matibabu wa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Londiani, Collins Kipkoech alisema miili 18 imechukuliwa na jamaa kwa ajili ya maandalizi ya maziko katika nyumba zao huku msako ukiendelea na utambulisho katika hospitali tofauti zilizoshughulikia majeruhi.
Alisema watu 49 walifariki katika hospitali ya Londiani, wawili waliaga dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho Jumamosi huku mwingine mmoja alifariki katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Rift Valley mjini Nakuru na kufanya jumla ya vifo kutokana na ajali ya Ijumaa jioni kufikia 52.
Kipkoech alisema miili saba kati ya waliotambuliwa inasubiri kufanyiwa uchunguzi kabla ya kutolewa kwa jamaa zao huku 12 wakiwa hawajatambuliwa.
Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen ametoa maagizo mapya baada ya ajali hiyo ya barabarani Londiani.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Murkomen alitoa wito kwa mashirika husika kurekebisha viwango vya mwendo kasi katika eneo hilo na kutoa matuta na alama.
Alisema masoko yote kando ya hifadhi ya barabara yahamishwe.
Murkomen alisema Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa kushirikiana na NTSA kuimarisha shughuli za kupambana na ulevi nchini kote.
Aliagiza Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama na Uchukuzi (NTSA) kujumuisha sehemu hiyo hatari kuwa mojawapo ya maeneo hayo.