Seneta wa Nandi Samson Cherargei amependekeza kuongezwa kwa muhula wa urais hadi miaka saba kutoka miaka mitano ya sasa.
Katika pendekezo yake iliyowasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo mnamo Ijumaa, Septemba 22,Cherargei anataka sheria ya sasa ya mihula miwili ya miaka mitano irekebishwe ili kusukuma idadi ya miaka ambayo mtu anaweza kutumikia hadi miaka saba katika kila muhula.
Hili, Seneta Cherargei anasema, lingempa rais muda wa kutosha kutekeleza manifesto yao.
“Kwa kuwa katiba ya sasa inatoa ukomo wa mihula miwili ya urais inayojumuisha miaka kumi, kuna haja ya kuongezwa kwa mihula miwili ya miaka saba kila moja. Hii inamwezesha rais kupata fursa nzuri ya kuunda na kuanzisha timu ya kutekeleza ajenda yake. ,” alisema Cherargei
Kulingana na seneta huyo, nyongeza hiyo pia itasaidia kukabiliana na changamoto za kudumu za uchaguzi nchini.
“Uchaguzi wa urais wa Kenya kila mara huwa na sifa kubwa kutokana na kuendeshwa kwa muda mfupi na hivyo kuufanya kuwa tukio la kufa kupona. Pia muda wa Miaka saba litamsadia rais kupanga serikali yake kwa minajili ya kutoa huduma kwa wananchi vilivyo” Alisema Cherargei.
Ikiwa pendekezo la Cheragei litatimia, itamaanisha kwamba kiongozi wa Kenya anaweza kuhudumu kwa jumla ya miaka 14 kwa urais wa mihula miwili.
Katiba kwa sasa inatoa muhula wa miaka mitano na usiozidi mihula miwili, ikimaanisha kuwa mabadiliko yoyote ya mfumo wa katiba yatahitaji kura ya maoni.