Baba, 65, Atupwa Miaka 30 Jela Kwa Kosa La Ubakaji Songwe.

Mahakama ya Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe imemhukumu kifungo cha miaka 30 Simon Salati Mwakasula (65) Mkazi wa Saza Wilaya ya Songwe baada ya kumkuta na hatia ya kosa la kumnajisi mwanafunzi wa darasa la tano shule ya Msingi Chato mwenye umri wa miaka 10.

Upande wa mashtaka katika shauri hilo umeeleza kuwa mtu huyo alitekeleza kitendo hicho Februari 09, 2024 kwa kumbaka mwanafunzi huyo baada ya kumlaghai kwa kumpatia zawadi ya soda kisha kwenda naye shambani kwake ambako alimbaka.

Shauri hilo limesikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Songwe Lefi Mathias Sizya likiendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Paschal George Manawa ambapo upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano ambao wameelezwa kuthibitisha kosa hilo dhidi ya mtuhumiwa ambaye ametiwa hatiani bila kuacha shaka kama sheria inavyoelekeza.

Mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Songwe Lefi Sizya, Mahakama imemhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka ili iwe fundisho kwake na watu wengine katika jamii.