Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Kanali aliyehusika na mauaji ya halaiki Rwanda aaga dunia. - Mwanzo TV

Kanali aliyehusika na mauaji ya halaiki Rwanda aaga dunia.

Theoneste Bagosora, Kanali wa zamani wa jeshi la Rwanda

Theoneste Bagosora, Kanali wa zamani wa jeshi la Rwanda aliyefahamika kwa kuchangia na kupanga mauaji ya kimbari ya 1994 ambapo Watutsi 800,000 na wahutu waliojaribu kuwalinda waliuawa, ameaga dunia hospitalini Mali.

Mwanawe Achille Bagosora , ametangaza kifo chake katika ukurasa wa Facebook. Bagosora alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 35 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mahakama ya kimataifa ya jinai ya Rwanda. Bagosora, mwenye umri wa miaka 80, alikuwa amehukumiwa kifungo cha maisha mnamo 2008 lakini baada ya kukata rufaa adhabu yake ilipunguzwa hadi miaka 35 gerezani.

Alijulikana kama mtu mwenye misimamo mikali alipokuwa kwenye Chama cha Kitaifa cha Demokrasia na Maendeleo chake Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana. Bagosora mnamo mwaka wa 1993, aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa baraza la mawaziri katika wizara ya ulinzi na akachukua udhibiti wa mambo ya kijeshi na kisiasa nchini humo.

Nafasi hiyo ilimpa uwezo mkubwa katika serikali, na alijibu tu kwa rais . Rais Habyarimana alipouawa katika ajali ya ndege, Bagosora alichukua uongozi wa nchi na kuamuru mauaji ya wa Tutsi. Baada ya mauji hayo ya kimbari, Bagosora alitorokea uhamishoni Cameroon. Alikamatwa mnamo 1996 na kusafirishwa hadi Arusha, Tanzania mwaka wa 1997. Usikilizaji wa kesi yake ulianza 2002 na kuendelea hadi 2007.

Bagosora alipatikana na hatia kwa kuhusika katika mauaji ya walinda amani 10 wa Ubelgiji na kuhusika na vifo vya waziri mkuu wa Rwanda na mkuu wa korti ya katiba.Alipatikana pia na hatia ya kuhusika kwa mauji ya Watutsi katika maeneo tofauti ya mji mkuu wa Kigali na Gisenyi magharibi mwa nchi.

Baada ya kupata habari za kifo cha Bagosora, Balozi wa Rwanda nchini Uholanzi Olivier Nduhungirehe, amesema kuwa Bagosora hakujutia maovu yake.

“Sababu kuu ya Bagosora kutaka kuachiwa mapema ni hakuwahi kukubali mchango wake katika mauaji hayo ya kimbari,na hakuwahi kusikitishwa au kujutia maovu yake.”
Nduhungirehe alisema kwenye Twitter.

Maombi ya Bagosora kutaka kutolewa mapema yalikataliwa mapema mwaka huu, jaji akiamua kuwa hajabadilika.