Rais Ruto ateuwa Wanachama wa upinzani kuwa Mawaziri

Wanachama kadhaa wa ODM, wengine ambao wanahudumu kwa sasa kama wabunge, wameteuliwa na Rais William Ruto kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri.

ODM  inaongozwa na kiongozi wa upinzani kenya Raila Odinga

Walioteuliwa ni pamoja na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Opiyo Wandayi ambaye pia ni Mbunge wa Ugunja. Wandayi ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati akichukua mahali pa Davis Chirchir aliyehamishiwa Wizara ya Barabara na Uchukuzi.

Mbunge mteule John Mbadi ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Fedha na mipango ya kitaifa , wadhifa ambao awali ulishkiliwa na Prof. Njuguna Ndung’u.

Magavana wawili wa zamani ambao ni wanachama wa ODM pia nao wameteuliwa kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri.

Wao ni aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika huku aliyekuwa Gavana wa Mombasa akiteuliwa kuwa Waziri wa Madini. Simon Chelugui ndiye aliyekuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika katika Baraza lililovunjwa la Mawaziri huku Salim Mvurya akiwa Waziri wa Madini. Mvurya sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara huku Chelugui akipoteza wadhifa wake.

Kumekuwa na hali ya kuvuta ni kuvute katika chama cha ODM juu ya ikiwa wanachama wa chama hicho wanastahili kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri au la.

Jana Jumanne, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema chama hicho hakina mipango ya kujiunga na serikali ya Rais William Ruto, msimamo ambao ulipingwa vikali baadhi ya wabunge wa Chama hicho

Isipokuwa ODM, vyama tanzu vya Azimio vikiongozwa na Kalonzo Musyoka wa Wiper vilipinga vikali wanachama wa muungano huo kujiunga na serikali ya Ruto.

Inasubiriwa kuona hatima ya muungano huo ikizingatiwa kwamba kiongozi wake Bw. Raila Odinga ameridhia wanachama wake kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri.