Rais Ruto amteua Dorcas Oduor Kuwa Mwanasheria Mkuu

Rais wa Kenya Dkt William Ruto amteua Dorcas Agik Oduor kuwa Mwanasheria mkuu wa Kenya

Iwapo ataidhinishwa na bunge Dorcas Agik Oduor atakuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kenya

Oduor, ambaye kwa sasa anahudumu kama Katibu wa Mashtaka ya Umma katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), ni wakili wa Mahakama ya Juu mwenye Shahada ya Uzamili ya Kudhibiti Migogoro ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Shahada ya sheria kutoka chuo hicho.

Kabla ya uteuzi wake, Oduor alishikilia nyadhifa mbali mbali katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya ODPP ikiwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi, Mkuu wa Idara ya uhalifu wa kiuchumi, kimataifa, Naibu mwanasheria mkuu wa serikali, na Wakili wa serikali katika ofisi ya mwanasheria mkuu.

“Wakili Mkuu Oduor amedhihirisha uadilifu , umahiri wa kitaalamu na kujitolea kwa uthabiti kwa utawala wa sheria. Iwapo ataidhinishwa na Bunge la taifa, Dorcas Agik Oduor atakuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwanamke katika taifa letu,” taarifa ya Ruto kwa Baraza la Mawaziri, iliyoandikwa na Mkuu wa Wafanyakazi katika ofisi ya rais, Felix Koskei imeeleza.

Uteuzi wake ni sehemu ya mabadiliko ya viongozi wa juu wa serikali yanayofanywa na Rais Ruto na baada ya kuwateua baadhi ya mawaziri kufuatia maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali yaliyosababishwa kufutwa kwa baraza la mawaziri.