Polisi walikuwa wamezingira barabara zinazoelekea gereza mapema asubuhi, waandishi wa habari wa AFP waliokuwa kwenye eneo la tukio waliona.

Sababu za wafungwa hao kutaka kutoroka kutoka gereza la Makala katika mji mkuu wa Kinshasa bado haijulikani wazi.

“Kuna jaribio la kutoroka katika gereza kuu la Makala. Huduma za usalama tayari zimerudishwa na hali ni tulivu na salama,” msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema Jumatatu kwenye X.

“Hali imedhibitiwa,” Muyaya aliiambia Televisheni ya Taifa ya DRC kutoka Beijing, ambako Rais Felix Tshisekedi yupo kwenye mkutano China na Afrika wiki hii.

Wakati mashahidi wakisimulia kusikia milio ya risasi, mamlaka haijatoa takwimu au taarifa yoyote kuhusu wafungwa waliofanikiwa kutoroka.

Daddi Soso, fundi wa umeme mwenye umri wa miaka 40 anayeishi katika eneo hilo, aliambia AFP kuwa aliamka usiku na kusikia milio ya risasi.

“Kulikuwa na milio ya risasi kuanzia saa saba au nane za asubuhi na hadi saa kumi na moja asubuhi,” Soso alisema, akionekana kutetemeka. “Kulikuwa na vifo, na kuna watu walikimbia,” alisema na kuongeza aliona magari ya sheria yakisafirisha miili.