Petroli yashuka bei Tanzania

Kulingana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA), gharama Petroli, Dizeli na Mafuta ya taa zimeshuka kwa asilimia 3.6, ukilinganisha na ilivyokuwa kwa mwezi Agosti.
Watumiaji wa nishati petroli nchini Tanzania wamepata nafuu baada ya punguzo la gharama za bidhaa hiyo muhimu.

photo courtesy/ Getty Images

Kulingana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA), gharama Petroli, Dizeli na Mafuta ya taa zimeshuka kwa asilimia 3.6, ukilinganisha na ilivyokuwa kwa mwezi Agosti.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Mwainyekule inaonesha kuwa watumiaji wa nishati ya petroli kwa mkoa wa Dar es Salaam, watalipia Dola 1.16 (Shilingi za Kitanzania 3,140) kwa mwezi Septemba, kutoka Dola 1.20 (Shilingi za Kitanzania 3,231)kwa mwezi Agosti.

Kwa upande wake, bei ya mafuta ya dizeli imeshuka kutoka Dola 1.15 (Shilingi za Kitanzania 3,131) hadi Dola 1.11(Shilingi za Kitanzania 3,011) kwa watumiaji wa mkoa wa Dar es Salaam.

“Kwa bei za Septemba 2024, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 0.91,” taarifa hiyo imesema.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166.

Pia, imevitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika