Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeanza kampeni yake ya kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa sare ya 0-0 dhidi ya Ethiopia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa kundi H, ambao ulitarajiwa kutoa ishara ya mwanzo ya matarajio ya Stars kwenye mbio za kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa ya soka barani Afrika.
Licha ya kuanza mchezo kwa shauku kubwa, Taifa Stars ilishindwa kutumia nafasi walizopata mwanzoni mwa mchezo. Timu ilionekana kujitahidi kushambulia, lakini ukosefu wa utulivu karibu na lango la Ethiopia uliwanyima nafasi za wazi za kupachika mabao.
Hasa katika kipindi cha kwanza, washambuliaji walishindwa kulenga lango ipasavyo, jambo lililowapa wapinzani muda wa kujipanga vizuri.
Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Taifa Stars ilifanikiwa kupiga mashuti matatu tu, yote yakiwa hayakulenga lango la Ethiopia. Walinzi wa Ethiopia walionekana kuwa makini katika kuhakikisha Stars hawapati nafasi ya kufunga, huku kipa wa Ethiopia akionekana kuwa katika kiwango bora.
Licha ya changamoto kwenye safu ya ushambuliaji, safu ya ulinzi ya Taifa Stars iliyokuwa ikiongozwa na kipa Ally Salim ilionyesha uimara mkubwa. Walifanikiwa kuzuia mashambulizi ya Ethiopia, ambayo mara kadhaa yalitishia kuzaa bao.
Mchezo wa Taifa Stars katika kipindi cha kwanza ulionekana kupungua kasi katika eneo la kiungo. Feisal Salum, Himid Mao, na Novatus Dismas walionekana kushindwa kuhimili kasi ya Ethiopia, hasa kwenye eneo la katikati mwa uwanja.
Ethiopia ilitawala eneo hilo kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo liliwapa udhibiti wa mchezo kwa muda mrefu wa kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa matumaini mapya kwa Taifa Stars, huku wakiweka jitihada za kufungua safu ya ulinzi ya Ethiopia. Hata hivyo, uchezaji wao ulikosa ubunifu na harakati zao zilionekana kuzimwa kirahisi na safu ya ulinzi ya Ethiopia.
Kocha wa Taifa Stars alifanya mabadiliko muhimu katika kipindi cha pili kwa kuwaingiza Pascal Msindo, Mudathir Yahya, na Wazir Junior, ambao walibadilisha mwelekeo wa mchezo kwa kiasi fulani.
Mabadiliko haya yaliifanya Taifa Stars kuongeza kasi ya mashambulizi, na kufanikiwa kupata kona mbili ndani ya kipindi cha pili. Hata hivyo, uimara wa kipa na walinzi wa Ethiopia uliendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa Taifa Stars.
Sare hii ya 0-0 imeiweka Taifa Stars katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi H, wakifuata nyuma ya Ivory Coast, ambao wanatarajiwa kuwa wapinzani wao wa pili kwenye mechi ijayo.
Mechi hiyo itachezwa ugenini Septemba 10, ambapo Taifa Stars itakutana na Guinea nchini Ivory Coast. Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu zaidi, lakini Taifa Stars italazimika kuongeza umakini na mbinu za kushambulia ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu.
Hisani ya Habari forum